Tukipeleke Kiswahili Afrika Kusini, tujifunze namna ya kuandaa makongamano

NA CAESAR JJINGO

Huku nchi ya Afrika Kusini ikiazimia kuanza kufundisha Kiswahili kwenye shule za nchi hiyo, wadau wa Kiswahili kutoka nje na ndani Afrika Mashariki,  wanepania kufanya msururu wa makongamano ya Kiswahili. Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimekwisha kusambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii, makongamano hayo yataandaliwa katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki;  Kenya, Uganda na Tanzania. Makongamano hayo ni pamoja na kongamano la nne la Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (CHALUFAKITA), katika Chuo Kikuu cha St. Augustine, Mbeya (Tanzania-Bara).

Mkutano huo wa siku mbili kati ya Agosti 2-3 mwaka huu. Kongamano la pili ni la Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Karatina, Kenya, tarehe 8-9 Agosti, 2019.  Kongamano hilo ni la ishirini na mbili tangu CHAKITA kuasisiwa mnamo 1998. Aidha, Kongamano la Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA), litafanyika katika Chuo Kikuu cha Masaai Mara, Narok, Kenya, kati ya tarehe 7 na 8 Novemba,  2019.  

Nalo Kongamano la  tano la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), litakafanyika katika Chuo Kikuu cha Kyambogo, Uganda, mnamo Desemba 13-15 mwaka huu. Pazia la msururu wa makongamano hayo litateremshwa na  kikao cha tatu cha Kongamano la Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), kitakachofanyika Zanzibar (Tanzania-Visiwani), mnamo Desemba, 19-20, 2019.  

Tathmini ya jicho kali inaonesha kwamba ndani ya Agosti 2019, kutakuwa na makongamano mawili – ya CHAKITA na CHALUFAKITA. Vivyo hivyo, mwezi wa Disemba, kutakuwa na makongamano ya BAKIZA na CHAUKIDU. Ni mwezi wa Novemba tu ambao utakuwa na kongamano moja la CHAKAMA. Tathmini ya maeneo ya kiojiografia inabainisha kwamba ndani ya eneo moja (Tanzania), kutakuwa na makongamao mawili: BAKIZA na CHALUFAKITA, na mengine mawili  yataandaliwa nchini Kenya  mathalan CHAKAMA na CHAKITA. Kutakuwa na kongamano moja tu nchini Uganda – CHAUKIDU.

Taswira ninayoichora hapa  ni kwamba ni vigumu kujua vigezo ambavyo watayarishaji wa makongamano haya walivitumia hasa ukizingatia kuwa wahudhuriaji wanatarajiwa kuwa ni walewale. Wataalamu wa Kiswahili Afrika ya Mashariki na Kati sio wengi mno kiasi cha kuweza kugawanywa katika makundi mbalimbali ili kuweza kuhudhuria makongamano yanayofanyika sambamba na sawia – katika maeneo tofauti ila yanayokaribiana kijiografia takribani ndani ya muda mmoja. Isitoshe, wakereketwa wengi wa Kiswahili wanaotarajiwa kuhudhuria vikao hivyo hujifadhili.

Kadhalika, mada ndogo zitakazoshugulikiwa kwenye makongamano haya zinakariabiana kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa pia na mwingiliano fulani. Tunapaswa tukumbuke kwamba tunashindwa kuelewa kimsingi vigezo vinavyotumika kuandaa makongamano. Vyama au mabaraza/ mashirika mbalimbali huwa na  malengo yao mahususi yaliyochangia kuanzishwa kwao. Aidha asasi zenyewe zina sababu tofauti za kuandaa haya makongamano.

Tofauti na ilivyo nchini Afrika Kusini, ijapokuwa vyama vyao vya lugha vina malengo tofauti (hasa vile ambavyo mwandishi wa makala haya amepata fursa kujumika navyo), ukifika muda wa kuandaa makongamano ya kitaaluma kama tunayoyatarajia mwaka huu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, viongozi wa vyama hivyo (vya Afrika Kusini) huja kwa pamoja ili kutekeleza (ma)jukumu yaliyo nje ya vyama vyao binafsi ila yenye uwiano na malengo ya vyama hivyo.

Kwa mfano, mnamo 2016, mwandishi wa makala haya alipata fursa ya kuwasilisha makala yenye mada “Task-based syllabus design with reference to reasoning tasks in teaching Kiswahili as second language in Ugandan secondary schools” kwenye kongamao la pamoja lililoandaliwa na vyama vitatu ambavyo kwa kifupi vinaandikwa kama ifuatavyo, LSSA, SAALA, SAALT. Kongamano hili liliandaliwa katika Chuo Kikuu cha Western Cape, kilichopo kwenye Rasi ya Magharibi, nchini humo. Kadhalika, kongamano lao la mwaka 2017, liliandaliwa na vyama vyote vitatu, kwenye Chuo Kikuu cha Rhodes, kilichopo Grahamstown, Afrika Kusini. Hususani, mwaka huu, kongamano lao limeandaliwa na vyama viwili tu. Yaani, SAALT & SALALS, litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Pretoria (tawi la Groenkloof), mnamo Juni, 30  hadi Julai 4,  2019.

Endapo jukumu  na azma yetu katika siku za usoni ni kukiendeleza Kiswahili, ipo  haja ya ‘kujifunza’ kutoka kwa wenzetu  wa Afrika ya Kusini. Kwanza, tuandae makongamano ya pamoja hasa iwapo maeneo yetu ya kijiograpfia yanakaribiana. Kwa mfano makongamano ya BAKIZA na CHALUFAKITA yangeunganishwa.

Ni jukumu la kamati ya maandalizi au waandaji kukubaliana  kuhusu vitovu  ambavyo vitakuwa rahisi kuwakongamanisha  wadau wao. Vilevile kwa kuwa makongamano ya CHAKITA na CHAKAMA yanatarajiwa kufanyika nchini Kenya, haya nayo yangeunganishwa pia na  kamati husika, katika kitovu kimoja.

Pia,  ipo haja ya kutathmini upya wakati mwafaka ambao utawaruhusu wahudhuriaji kuweza kuhudhiria makongamano yalioandaliwa. Kwa hiyo ninapendekeza makongamano yawe ya pamoja na yaandaliwe hasa pale vyuo vingi vikiwa likizoni. Aidha, iwe katikati ya au mwishoni mwa mwaka.

Lengo kuu ni kuwapa fursa wahudhuriaji kujiandaa  – hasa kifedha ili kuweza kusafiri  na kuhudhuria  makongamano (kama itawezekana yote) ya mwaka husika bila kusumbuka. Isitoshe, endapo makongamano yatakuwa machache, hata ufadhili unakuwa rahisi kupatikana kutoka kwenye vyuo vyetu husika hususani vile vya kibinafsi. Ikiwezekana pia,  si lazima kila mwaka vyama husika viandae makongamano.Viongozi wa vyama vya Kiswahili wanaweza kukubaliana kwa mfano kila baada ya miaka miwili vyama fulani vitaandaa kongamano  fulani kwa zamu ya mzunguko nakadhalila.

Dkt Caesar Jjingo ni mhadhiri msaidizi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.

Baruapepe; caesarial@gmail.com

Author: Gadi Solomon