UCHAMBUZI WA VITABU TAHINIWA VYA FASIHI: Maudhui katika Tamthilia ya ‘Kigogo’

Na WANDERI KAMAU

Nafasi ya mwanamke

BAADHI ya wahusika wanawake katika tamthilia hii wamesawiriwa kuwa wazalendo na mashujaa, huku wengine wakiibukia kuwa wasaliti na adui za wao kwa wao.

Sera ya uongozi katika jimbo hili pia inaonekana kuwatenga wanawake, ndiyo sababu baadhi yao kama vile Tunu wanaibukia kuwa wapiganiaji ukombozi.

Sudi anapochonga kinyago cha shujaa mwanamke, Kenga anamwambia kuwa Sagamoyo haijawahi kuwa na mwanamke ambaye ni shujaa. Katika historia ya jimbo hilo, wanawake wamekuwa wakitengwa kabisa katika masuala yanayohusu uongozi (uk10).

Kenga anasema kuwa kinyago hicho hakitanunuliwa, ambapo anabadilisha mawazo yake na kusema kuwa afadhali achonge kinyago cha ngao.

Kimsingi, tukio hili linaonyesha dhana hasi iliyo katika nafsi za Wanasagamoyo wengi, kwamba mwanamke hana uwezo wowote, hasa kuhusu masuala ya uongozi.

Wanawake pia wanasawiriwa kuwa washerati (mahawara). Kwa mfano, Sudi anapokataa kuchonga kinyago, Kenga anamwambia kuwa “amelishwa kiapo na hawara wake” (uk12). Hili linaashiria udhalilishaji wa mwanamke na jamii.

Wanawake vilevile wanachukuliwa kama mapambo katika jimbo hilo, kuonyesha kwamba hawana thamani yoyote.

Majoka anamwambia Ashua kuwa urembo wake hauwezi kufananishwa na lolote.

“…nikufananishe na nini? Urembo wako hauna mfanowe Ashua” (uk20).

Majoka anamshauri Ashua atumie urembo wake vizuri kwa kuwa ni wa muda tu (uk25).Wanawake wenyewe wanaonekana kukubali kudhalilishwa kwao, kwani Husda anakubali dhana kuwa wanawake ni kama mapambo tu (uk6).

Wanawake wanasawiriwa kuwa wenye maringo, kwani Majoka anasema Ashua alikataa kazi ya ualimu kutokana na maringo yake (uk 25).

Wanawake wanaibukia kuwa maadui wa wenyewe kwa wenyewe. Kwa mfano, Husda anamwita Ashua kuwa mdaku, kimada wa kuwinda waume wa watu, licha ya nia yake kutokuwa hivyo.

Uongozi mbaya

Jimbo la Sagamoyo linakumbwa na msururu wa migomo na maandamano ya wafanyakazi.

Wauguzi wa Sagamoyo wanaandamana. Walimu wa Sagamoyo pia wanagoma wakiwa likizoni kwa kutolipwa mishahara yao.

Hali hii inaendelea katika jimbo hili kuashiria jinsi uongozi wa Majoka umewatelekeza wafanyakazi kwa kutoshughulikia maslahi yao.

Katika kiwanda cha Majoka and Majoka Company, anakofanya kazi Siti, watu wanagoma kwa kutolipwa mishahara. Vijana watano wanauawa katika harakati za kuitisha mishahara yao.

Hali pia ni tete katika Soko la Chapakazi, ambako wachuuzi wanaandamana wakilalamikia sera mbaya za uongozi wa Sagamoyo na usimamizi wa soko hilo. Baadhi yao wanaumizwa.

Wachuuzi hao wanalalamikia hatua ya uongozi wa Majoka kulifunga soko hilo.

Hali ya maandamano jimboni humo inaonekana kuwa jambo la kila siku, kwani magazeti hayakosi kuwa na picha za watu wakiandamana.

Katika mojawapo ya habari iliyo magazetini, Tunu anaonekana akiongoza maandamano miongoni mwa watu wanaojiita wanaharakati (uk32).Anapowahutubia wanahabari, Tunu anaulaumu uongozi wa Majoka kwa kufuja pesa zilizopaswa kutumiwa kulisafisha soko hilo. Pesa hizo zinafujwa, jambo linalowakasirisha sana wachuuzi. Anasema kuwa uongozi huo unalifunga soko badala ya kulisafisha (uk32)

Kwa habari zaidi soma>>>>https://taifaleo.nation.co.ke/?p=38455

Author: Gadi Solomon