UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya utafiti kidijitali katika ukuaji, maendeleo ya Kiswahili

Na MARY WANGARI

KATIKA siku za hivi karibuni, wadau kadha wa Kiswahili wamejitokeza kulipigia debe suala la Kiswahili kuwa lugha rasmi si tu Kenya, bali pia Afrika Mashariki kwa jumla.

Juhudi hizi zinapaswa kupongezwa na pia zinapaswa kuwa mwamko mpya kwa wadau wa Kiswahili kutilia maanani teknolojia ili kuimarisha nafasi ya lugha hii katika kizazi cha sasa. Kwa mintarafu hiyo, ni muhali kupuuza nafasi ya teknolojia katika ukuzaji na maendeleo ya Kiswahili ili kuweza kukidhi mahitaji ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika karne hii.

Utafiti wa kidijitali pamoja na lugha mitandaoni ni baadhi ya masuala mapya ambayo yana nafasi muhimu mno si tu kwa lugha za Kiafrika kama vile lugha ya Kiswahili, bali pia lugha za kimataifa. Hii hasa ni kwa kuwa utafiti wa kidijitali au lugha ya kimtandao inafidia mapungufu yanayoshuhudiwa katika utafiti kimapokeo au utafiti wa king’amuzi (Intuitive Research).

Kuna sera kadha wa kadha zinazoimarisha Teknolojia ya Lugha, hali inayoipa nafasi muhimu kwa lugha zinazotimiza majukumu nyeti kimawasiliano. Teknolojia ya lugha inatoa nafasi kwa Lugha za Kiafrika ambazo hazijapata fursa ya kuwepo katika jukwaa la kidijitali kwa muda mrefu kama baadhi ya lugha zenye asili ya Ulaya zilivyo, pia zinatafitiwa na kuainishwa kwa kutumia teknolojia ya lugha angalau kwa kiwango kidogo sana. Kama wanavyohoji wataalamu De Pauw et al (2006) De Pauw and de Schryver (2008) na wengineo, Kiswahili ni mojawapo wa lugha za Kiafrika ambazo zimedhihirisha uwapo mkubwa kwenye majukwaa ya kidigitali. Isitoshe, katika majilio ya intaneti, lugha kadha za Kiafrika pia zimejikuta katika mazingira haya ya kidijitali-mtandaoni.

Ni wazi kuwa ndio kwanza mkoko unaanza kutoa maua katika utafiti wa dijitali au ukipenda matumizi ya teknolojia katika Kiswahili pamoja na lugha nyinginezo za Kiafrika ikilinganishwa na lugha za mataifa yaliyoendelea kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kijapani, Kichina, Kijerumani, Kireno miongoni mwa nyinginezo.

Maendeleo katika utafiti kidigitali yamepiga hatua kwa kiasi cha kuzuka kwa Maarifa Kimtandao

Mosi, mfumo wa mawasiliano kwa kutumia kompyuta uliozuka kwa kasi katika uwanja wa teknolojia na kubadilisha pamoja na kurahisisha utendajikazi kwa njia ambayo hata isingeweza kufikiriwa. Ni vyema kufahamu kuwa kumekuwa na juhudi kadhaa za utafiti wa Kiswahili kwa kutumia teknolojia ya lugha kutoka kwa wanaisimu na wataalamu mbalimbali wa Kiswahili. Baadhi ya tafiti hizi zimeangazia Kiswahili kwa kuchunguza viambajengo vyake mbalimbali. Tafiti hizi kidigitali hutumia programu aghalabu hujikita kwenye kanuni za lugha na zile za kimtandao au ukipenda kikompyuta.

Kuna mbinu mbalimbali zinazohusika katika utafiti wa lugha ya Kiswahili kidijitali zinazoambatana na vipengele mbalimbali vya lugha. Dhamira kuu ya utafiti wa Kiswahili kidijitali ni kukuza na kuendeleza Kiswahili kama lugha muhimu ya Kafrika kupitia Uhandisi wa Lugha au Teknolojia ya Lugha.

NADHARIA: Baadhi ya nadharia muhimu zinazotumika katika mchakato wa utafiti wa Kiswahili kidigitali ni pamoja na Nadharia ya Isimu Kongoo au Mtazamo wa Kikongoo na Nadharia ya Msambao wa Uvumbuzi (Diffusion of Innovation Theory) ambayo mwasisi wake ni Everett Rogers (2003). Lengo kuu la mikabala hii ni kujaribu kufafanua jinsi utafiti kidigitali ulivyo na manufaa zaidi katika kizazi cha leo ikilinganishwa na utafiti kwa kutumia mitindo ya kimapokeo.

MANUFAA: Aidha, tafiti za wataalamu kadha waliolivalia njuga suala hili, zimehitimisha kuwa utafiti wa lugha kidigitali una manufaa mengi ikizingatia kuwa mitambo au tarakilishi zina uwezo mkubwa zaidi wa kukusanya na kuchakata data ikilinganishwa na binadamu. Kiwango kikubwa cha data inayokusanywa inampa mtafiti upeo zaidi wa utafiti, utafiti kidigitali huwezesha kuhifadhi data kimtandao hivyo kurahisisha mchakato wote wa utafiti kuanzia uundaji, tathmini kwa kujumuisha kamusi, tafsiri-kimtandao uchanganuzi kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki,ufundishaji lugha na kadhalika.

Author: Amani Njoka