UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uigaji hauzuiliki katika ubunifu hasa wa kazi za fasihi

Na Enock Nyariki

KATIKA ubunifu wa kazi za fasihi – novela, riwaya, tamthilia au hadithi fupi – mwandishi hujikuta amemuiga mwandishi au waandishi wa kazi fulani.

Jambo hilo hutokea hivyo kusudi au hata bila kukusudiwa. Hata hivyo, haitakuwa sahihi kusema kuwa yupo mwandishi mmoja ambaye hakuathiriwa na kazi za mtunzi au watunzi wengine.

Vivyo hivyo, hayupo mwandishi aliyefanikiwa katika uandishi wake bila kuzisoma kazi za wengine. Uandishi mzuri hutokana na usomaji mpana wa kazi za watunzi wengine. Usomaji huo haukamiliki pasi na kuathiriwa na kazi hizo.

Waandishi huathiriwa na wengine kwa njia mbalimbali. Huathiriwa katika matumizi ya msamiati.

Baadhi ya maneno huenda si mapya lakini watangulizi huwa wameyatumia kwa namna fulani waliyoipendelea wenyewe.

Mfano mzuri ni wa matumizi ya neno ‘shangazi lake’ au ‘shangazi langu’ katika baadhi ya kazi za Shaaban Robert – mfano mzuri ukiwa ule wa ‘Siku ya Watenzi Wote’. Kimsingi, kivumishi kimilikishi na cha A-unganifu cha neno hilo shangazi kingetarajiwa kuwa ‘yangu’ na ‘ya’ katika mfuatano huo. Hata hivyo, Shaaban Robert, kwa sababu yake mwenyewe, ameamua kutumia ‘shangazi langu’ na ‘shangazi la’.

Profesa Ken Walibora, katika riwaya yake ya awali ya ‘Siku Njema’ anaelekea kutekwa sana na matumizi ya ‘shangazi langu’ na ‘shangazi la’ jinsi yanavyojitokeza katika kazi ya Shaaban Robert.

Ijapokuwa mtu hawezi kudai umiliki wa msamiati fulani wa Kiswahili, namna ya kuutumia msamiati huo inaweza kuonyesha uigaji wa aina fulani.

Kwa mfano Profesa Said A. Mohamed ana mazoea ya kutumia neno ‘danda’ lenye maana ya kuenea au kukolea kwa kitu. Neno hili linajitokeza katika baadhi ya kazi za Shaaban Robert.

Uigaji mwingine hujidhihirisha kwa njia ya mtindo. Waandishi wanaweza kuigana kwa namna wanavyounda sentensi zao.

Profesa Said A. Mohamed anaelekea kuazima vipengele fulani vya kimtindo kutoka kwa Mohamed S. Abdulla.

Waandishi wote wawili wanayo namna fulani ya kuanza na kumaliza sentensi zao ambayo inaelekea kulingana kwa namna fulani.

Wote hutunga sentensi fupi zinazoanguka kwa makurubundi ya risasi. Kazi za Ben Mtobwa vilevile zinaelekea kuathiriwa na zile za marehemu Mohamed S. Abdulla kimtindo.

Uigaji mwingine huwa ni wa wahusika na uumbaji wa wahusika. Ingawa hapana mwandishi yeyote anayeweza kudai umiliki au ukiritimba wa majina hususan majina ya Waswahili, jinsi ya kuwaumba wahusika inaweza kuwafanya waandishi wawili kushabihiana kwa namna fulani.

Katika kazi ya Shaaban Robert ya ‘Wasifu wa Siti Binti Saad’ mwandishi anaelekea kumpa mhusika Siti Binti Saad sifa zenye upekee – sifa za kimalaika.

Wapo waandishi wengine ambao japokuwa wahusika wao ni tofauti sana kimajina, wamepewa sifa hiyo ya kimalaika inavyojitokeza katika diwani ya Sheikh Shaaban Bin Robert.

Soma zaidi>>> https://taifaleo.nation.co.ke/?p=43782

Author: Amani Njoka