Vitabu vya Watanzania, kwa Watanzania viandikwe kwa Kiswahili kwanza

Nianze kwa kupongeza kazi nzuri za uandishi wa vitabu kadhaa ambavyo vimeandikwa na waandishi mbalimbali kuelezea maisha yao binafsi na ya kijamii jambo ambalo linatoa hamasa kwa watu wengi pale ambapo vitabu hivyo vitasomwa hasa ukizingatia umashuhuri, umaarufu na ushawishi wa watu hao kwa jamii. Kwa kweli ni jambo la kupongeza sana. Uandishi huu ni muhimu kwani wasomaji hupata maarifa na kufahamu mbinu mbalimbali, changamoto na mafanikio ya waliyoyapa watu hao. Waandishi hawa wamejitahidi kwa kadri ya uwezo wao kutoa kile walichonacho kwa kutumia lugha iliyokuwa rahisi kwao.

Ni ukweli usiopingika kwamba lugha ni mhimili mkubwa kwa jamii yoyote. Ni msingi wa maelewano, utangamano na uhamishaji wa maarifa na taarifa kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine. Kwahiyo ili mtu aweze kuyapata maarifa yaliyomo kwa mtu yawe ya kusemwa au kuandikwa, ni lazima yawe katika lugha inayoeleweka.

Wakati taifa lipo katika mjadala wa kuyahamisha maarifa ya kitaaluma kutoka lugha za kigeni kuja katika lugha ambayo wanafunzi wanaifahamu na kuielewa vyema kuliko lugha za kigeni, ghafla tunapata maarifa mengine muhimu na makubwa yaliyowekwa katika maandishi  na Watanzania ambayo hayahitaji kutazama mtaala wala silabasi.

Ni jambo la kujiuliza, inakuwaje kitabu kilichoandikwa na Mtanzania kwa ajili ya jamii yake ya Watanzania kinaandikwa kwa lugha ya kigeni mathalani Kiingereza? Ni kina nani wamelengwa kunufaika na kitabu hiki? Kitabu hiki kilichoandikwa na Mtanzania kwa ajili ya Watanzania kutumia lugha ya Kiiingereza ni kujipa kazi nyingine ambayo haina ulazima wowote.

Tukirejelea mfano, kitabu cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Benjamin Mkapa kiitwacho My life, My purpose (Maisha yangu, Kusudi langu) kilichozinduliwa katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, licha ya kwamba ni kitabu kizuri kilichosheheni mambo lukuki ya maisha yake binafsi pamoja na urais wa nchi yetu, bado inaweza kuwa vigumu kupata maarifa yaliyomo mule kama alivyokusudia na mwandishi.

Kitabu kimesheheni safari ya milima na mabonde ambayo ameipanda na kushuka kama kijana wa Kitanzania, wa maisha ya kawaida kabisa na ya chini kama ambavyo Watanzania wengi tumepitia na tupo hivi leo. Ni kitabu hiki ndicho ambacho kitapaswa kurudi kwa vijana wengine wadogo walio katika vijiji vya ndani wanaotembea umbali mrefu kuitafuta elimu, ni kitabu hiki ndicho kinachotakiwa kisomwe na Watanzania ambao elimu yao ni ya kiwango cha kati na chini ili kupata motisha kutokana na yale aliyoyapitia Mzee wetu, Benjamin Mkapa.

Hata hivyo maarifa hayo yamewekwa katika lugha ambayo walio wengi, walio wa takaba la chini, vijana wa Kitanzania wenye ndoto za kufika pale alipofika Mzee wetu bila kujali kiwango chao cha elimu wahaielewi. Ni vipi mtoto wa shule ya msingi, wazazi wetu ambao kwa namna moja ama nyingine hawajaweza kukifahamu Kiingereza watapata maarifa haya adhimu, makubwa na yenye motisha kubwa kwa ajili yao na watoto wao? Ni vipi wazazi watawausia na kuwatia moyo watoto wao waongeze bidii katika masomo na hata uongozi kama Mh Mkapa ikiwa hawajayaelewa vyema yaliyoandikwa?

Miezi kadhaa iliyopita tulishuhudia kuchapishwa kwa kitabu kingine bora kabisa na kijana wa Kitanzania, mwana wa Kitanzania, Hayati Dk Reginald Mengi. Kitabu hiki ni kama cha Mh. Rais Mstaafu pia kimejaa simulizi za kusisimua, simulizi za kutia moyo, kuhamasisha, simulizi za kutisha na kuumiza lakini zinazompa mtu nguvu ya kuthubutu. Hakuna shaka kuwa Kitabu I can, I must, I Will (Ninaweza, Inanilazimu, Nitafanya), kiliandikwa kwa lengo la kuwajulisha Watanzania hasa vijana safari yake ya mafanikio na kuwatia moto. Hata hivyo kitabu hicho pia kiliandikwa kwa Kiingereza kabla ya kutafsiriwa.

Vitabu hivi vyote viwili vimetumia lugha ambayo kwa kweli si rafiki kwa Watanzania walio wengi, sasa maarifa haya makubwa yaliyopo katika vitabu hivi yataeleweka kwa Watanzania wangapi na wa matabaka yepi? Tuangalie vitabu hivi visiishie kuwanufaisha walio wasomi pekee.

Nionavyo mimi, ipo haja ya wana wa Watanzania, wazalendo ambao wana nia ya dhati kuyaandika maarifa na yale walio na uzoefu nayo kwa ajili ya Watanzania yawe yanaandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha ya Watanzania wote na Afrika Mashariki. Ni rahisi Watanzania wasio kifahamu vyema Kiswahili kuyaelewa maarifa hayo kuliko Watanzania wasiokifahamu Kiingereza ambao ni wengi zaidi.

Ninaunga mkono ombi la Mh. Rais Dk John Pombe Magufuli alilolitoa katika hotuba yake kwamba kitabu cha Mh. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kitafsiriwe kwa Kiswahili ili Watanzania walio wengi waweze kukisoma. Kuna umuhimu wa waandishi wetu kuona kwamba lugha ya wale anaowaandikia ni Kiswahili hivyo ni vyema wachague kwanza kuandika kwa kutumia Kiswahili kisha lugha nyingine zifuate kwani sioni haja ya Watanzania kuandika vitabu kwa lugha za kigeni ikiwa vitabu hivyo ni kwa ajili ya jamii wanayoiandikia. Tujifunze kwa mataifa ya wenzetu yanapoandika vitabu kwa lugha yao kisha vinatafsiriwa kwa lugha nyingine. Hii itawanufaisha zaidi walengwa wa vitabu hivi lakini pia waandishi wenyewe watauza vitabu vingi zaidi kwa kuwa wanunuzi watakuwa wengi na hivyo kupata faida.

Kwa kuwa vitabu kama hivi vya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Hayati Dk Mengi na vingine vinahusu maisha duni kabisa ya walio wengi, kuna haja ya kufanyika mapinduzi ya haraka kimtazamo kwa kuviandika vitabu kama hivi na kuvitafsiri katika lugha ya Kiswahili ili yale maarifa yaliyokusudiwa na waandishi wenyewe kuwafikia wale ambao hasa ni jamii iliyowakuza na waliyomo.

Kwa kutafsiri vitabu hivi vijana wadogo na wakubwa wazazi na walezi wataweza kupata maarifa muhimu ambayo ni faida kwa mustakabali wa maisha yao ya sasa na baadaye. Maarifa haya yataibua na kuongeza nguvu na motisha kwa Watanzania wote bila kujali matabaka ya kielimu.

Mwandishi ni mdau wa Kiswahili.

Simu: 0672395558

Baruapepe: amanizacharyson@gmail.com

Author: Gadi Solomon