MAKOSA KATIKA MATUMIZI YA BAADHI YA JOZI ZA MANENO YA KISWAHILI

Na Mwandishi Wetu

Makala yetu ya leo yanakusudia kujadili makosa katika matumizi ya baadhi ya jozi za maneno ya Kiswahili. Lengo ni kuonyesha namna ambavyo baadhi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakifanya makosa katika utumiaji wa jozi hizi. Lengo la pili ni kuonyesha matumizi sahihi ya jozi hizi ili kuondoa matumizi potofu na yaliyozoeleka kwa watumiaji wengi. Jozi hizi za maneno zimechaguliwa kutokana na kufanana kwake, mathalani, neno moja kuwa kinyume cha jingine au kutokana na kufanana kimaana na kimatumizi.

Neno ‘jozi’ kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili, Toleo la Pili, 2017 iliyoandikwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ni, “Seti ya vitu viwili aghalabu vinavyowiana, kufanana au kushabihiana.”

Mbali ya  Kamusi Kuu ya Kiswahili makala haya yatafafanua jozi zilizoteuliwa kwa kutumia kamusi nyingine kama vile Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la 3 (2013) iliyoandikwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia, marejeo mengine ya makala haya ni Kamusi ya Kiswahili fasaha (2010) iliyoandikwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Kamusi ya Karne ya 21, Toleo Jipya (2015) iliyochapishwa na Longhorn Publishers na Kamusi ya Visawe iliyoandikwa na Mohamed A. Mohamed na Said A. Mohamed.

Makala haya ni mfululizo wa makala nyingine zinazoendelea kuandikwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) katika gazeti hili. Ifahamike kuwa BAKITA liliundwa kwa Sheria Na. 27 ya Bunge ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1983 na 2016. Sheria hiyo inaelezea baadhi ya majukumu ya BAKITA kuwa ni kukuza maendeleo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili mahali pote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za Serikali na kwa shughuli za umma. Jukumu jingine ni kuhimiza matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili na kuzuia upotoshaji wake.

Hivyo, kwa kuzingatia majukumu ya hapo juu, ni wajibu wa BAKITA kuwakumbusha watumiaji wa lugha ya Kiswahili mara kwa mara pindi matumizi ambayo yanakiuka ufasaha na usanifu wa lugha yetu adhimu ya Kiswahili yanapojitokeza. Lengo ni kuelimishana ili tuendelee kuitumia lugha yetu ya Kiswahili kwa usanifu na ufasaha na pia kuendelea kuidumisha lugha hii ambayo ni moja ya tunu za Watanzania.

Aghalabu na Nadra

Tuanze na maneno Aghalabu na Nadra: Baadhi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili huyatumia maneno haya isivyo sahihi. Ifahamike tu kuwa neno Aghalabu maana yake ni mara nyingi, kwa kawaida au mara kwa mara. Maneno mengine yanayofanana na neno hili ni kwa desturi, zaidi, mno na hasa. Neno hili linapaswa litumiwe katika sentensi zinazozungumzia tukio linalotokea mara nyingi au kurudiwa mara kwa mara. Kwa mfano, ‘Aghalabu shule hufungwa mwezi wa sita na mwezi wa kumi na mbili’ au ‘Ukizingatia ushauri wa wataalamu wa afya Aghalabu utakuwa na afya njema.’

Nadra kwa upande wake ni kinyume cha Aghalabu. Maana ya Nadra ni kwa uchache au upatikanaji wa kitu usio wa mara kwa mara; upatikanaji wa shida. Maneno mengine yenye maana sawa na Nadra ni haba  na adimu. Nadra inapaswa itumiwe katika utokeaji usio wa mara kwa mara wa jambo. Nadra inaweza kutumiwa katika sentensi kama vile: ‘Ni nadra sana kwa mtu asiye na juhudi ya kazi kupata mafanikio’ au ‘Ni nadra sana kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupata mafuriko.’

          Ukwasi na Ukata

Tuangalie  jozi nyingine ya maneno ambayo ni Ukwasi na Ukata. Ukwasi maana yake, ni utajiri au hali ya kuwa na mali nyingi. Neno hili linapaswa litumiwe katika matendo au matukio yanayosababishwa na hali ya utajiri ya mtu. Mathalani, mtu anaweza kusema: ‘Ukwasi wake umemfanya anunue gari la kifahari’ au ‘Anaishi kwenye nyumba ya kifahari kutokana na ukwasi wake.’ Kinyume cha ukwasi ni ukata.

Ukata, ni hali ya mtu kutokuwa na fedha zinazoweza kumsaidia kukidhi mahitaji yake. Maneno mengine yenye maana sawa na ukata ni umaskini, ufukara na uchochole. Ukata unaweza kutumiwa katika sentensi mathalani, ‘Ameshindwa kulipa kodi ya nyumba kutokana na ukata’ au ‘Ukata umemfanya akubali kumuoza binti yake kwa nguvu.’ Kwa maelezo na mifano hiyo ya Ukwasi na Ukata tunatarajia kuwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili watazingatia ufasaha na usanifu huo.

      Mwathirika na Mhanga

Jozi ya tatu ni Mwathirika na Mhanga. Tukianza na Mwathirika, ni ama mtu anayepatwa na jambo linalomsababishia madhara bila yaye kukusudia au mtu anayefuata tabia na mienendo ya mtu mwingine. Hivyo, dhana hii inaweza kuwa na maana chanya au hasi. Wako watu walioathiriwa na mienendo na tabia nzuri za walimu wao, wazazi wao, walezi wao, marafiki wao na hata majirani wao. Hata hivyo, wako pia walioathiriwa vibaya kama vile na mafuriko, vita, uvamizi, ukame, tetemeko, magonjwa n.k. Katika matumizi mtu anaweza kusema, ‘Mwathirika yule wa mafuriko amepatiwa hema’ au ‘Juma ni Mwathirika wa tabia na mwenendo wa mwalimu Nehemia.’ Hapa tunakusudia kuondoa dhana mbaya iliyojengeka katika jamii yetu ya kuhusisha kuathirika na ugonjwa wa UKIMWI.

Mhanga kwa upande wake, tukiacha maana ya mnyama anayesifika kwa kuchimba na kuishi kwenye mashimo, ni mtu anayeyatoa maisha yake kwa ajili ya maslahi yake, kikundi, jamii au taifa lake. Mhanga hufanya hivyo kwa kudhamiria, na hii ndiyo tofauti kubwa kati yake na Mwathirika ambaye aghalabu hukumbwa na baa bila ya kutarajia. Katika matumizi inaweza kuwa: ‘Wahanga wawili wamepoteza maisha yao na ya wengine kadhaa baada ya kujilipua sokoni.’ Mfano mwingine unaweza kuwa, ‘Mhanga mmoja alikamatwa uwanja wa ndege akiwa amejifunga mabomu.’ 

Kisimbuzi na King’amuzi

Tuzungumzie pia Kisimbuzi na King’amuzi. Kisimbuzi ni chombo maalumu kinachotambua ishara zilizofichwa na kuzifanya zionekane au kusikika katika redio, simu au televisheni. Visimbuzi ndivyo tunavyovitumia katika televisheni majumbani mwetu. Kisimbuzi kimetokana na neno simba ambalo kinyume chake ni simbua. Kusimba ni kuelezea jambo kwa namna ya kificho kwa kutumia ishara na alama. Kinyume chake ni kusimbua yaani kubaini taarifa uliyopewa kwa njia ya kificho. Hivyo, kifaa kinachowezesha kubaini yaani kusimbua ni Kisimbuzi. Mfano wa matumizi unaweza kuwa, ‘Baba amelipia Kisimbuzi chetu ili tuone fainali za kombe la dunia’ au ‘Kisimbuzi chetu kilipoharibika tulikirudisha kwa wakala aliyetuuzia.’

Makala haya yameandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).

Author: Gadi Solomon