Mambo ya msingi kuzingatia unapotaka kuandika kitabu chako

Na Ismail Himu

Uandishi wa fashihi hasa tamthiliya na riwaya umekuwa ni sehemu ya maisha yangu kwa zaidi ya miaka kumi sasa na ninajivunia kwa hilo.

Miongoni mwa vitabu nilivyoandika ni tamthiliya ya CHANZO NI WEWE, USASA USASAMBU, NJIA IMEPATIKANA, WAKILIA TUTACHEKA na riwaya ya DIWANI HAYAWANI. Pia nina kitabu cha ushairi kiitwacho TUMAINI AFRIKA nilichoshirikiana na BERYA M. JASPER

Kwenye majukwaa mbalimbali ya waandishi ninayopita nakutana na makundi makubwa ya vijana wanaotamani kuandika au hata waliowahi kuandika vitabu lakini wakiwa na changamoto mbalimbali. Wapo wanaohoji, “Himu mbona mimi nimeandika lakini sioni manufaa ya kuandika kitabu?” Wengine wakiamini maisha niliyonayo labda ni faida ya vitabu ninavyoviuza jambo ambalo si kweli.

Sasa leo nimeona lazima niongee na vijana wenzangu wa Tanzania na wasio Watanzania wanaotaka kuanza kuandika vitabu au walioandika kwamba uandishi wa kazi za fasihi ni sanaa kama ilivyo sanaa nyingine. Jamii ikipokea utapata hela na jamii isipopokea inatakiwa uendelee na sanaa yako hata kama haupati pesa.  Umaarufu wa mwandishi wa vitabu unachukua muda mrefu tofauti na sanaa nyingine kama muziki. Subra, uvumilivu na ujasiri ndio vitakavyokuokoa katika hili.

Lazima tukubali kwamba anayependa pesa hatotosheka na pesa na anayependa mali hatotosheka nazo hata apewe ulimwengu mzima. Ipende sanaa yako ikikulipa shukuru na ongeza jitihada kwani ukiiacha Mungu ataondoa kipaji hicho na kumpa mwingine kwani kipaji ni neema ambayo Mungu hugawa kwa watu wake wote, atakayekiendeleza kitamnufaisha na atakaekipuuza atapokonywa na kupewa mwingine hivyo lazima tukitumie ipasavyo.

Changamoto kwenye uandishi ni nyingi sana tena sana lakini haimaanishi kwamba ndio tuache kuandika. Lazima kila siku utafute njia ya kukabiliana na changamoto hizo kama unavyokabiliana na changamoto nyingine za maisha. Hebu tazama baharini, dhoruba inapotokea unaweza ukadhani haitakata kumbe shwari ndio inakaribia.

Leo nimekuja na mambo muhimu Matano (5) ya kuzingatia ili uweze kumudu changamoto na misukosuko kwenye tasnia hii ya uandishi.

  1. NENO NITAFANYA, nitafanya ni neno dogo sana ambalo limeathiri maisha ya watu wengi hapa ulimwenguni, ili uweze kuwa mwandishi mzuri neno hili linatakiwa liondoke mdomoni mwako na ndani ya nafsi yako.

Ahairishaye mambo hukumbwa na kazi nyingi zisizokamilika baadaye. linalowezekana kufanya leo kwanini lingoje kesho? Pale wewe unaposema nitafanya kuna vijana wenzako ulimwenguni wanafanya kweli. Ukiamua kuandika andika hata kwa udogo wa maneno kumi.

Maslahi ya pupa: Pesa na mali ndio vitu vinayowashughulisha binadamu toka zama na zama, kwa mwandishi haswa waandishi wachanga napenda kuwaambia pesa sio jambo la kuwazia unapoanza kuandika, wewe andika sana. Acha maandiko yako yaingie kwenye nyoyo za watu uone pesa itakavyokuja yenyewe. Lakini ukiandika kitabu kimoja au viwili uanze kukata tamaa ya mauzo, hutoweza kuaendelea kuandika.

Tuige mifano ya wazee wetu waliotutangulia kwenye uandishi, waliandika kama sehemu ya maisha yao, waikomboe jamii yao lakini baadaye vitabu vikapata umaarufu na wao wakaanza kunufaika.

Jambo kubwa zaidi kwenye hili nawaambia tujitahidi kuacha alama kwenye jamii yetu, tusife tu kama kuku. Sisi tumepewa akili na utashi lazima vizazi vinavyokuja vitambue uwepo wetu kama sisi tunavyotambua uwepo wa waliotutangulia kupitia maandiko yao. Tujifunze kufanya kazi kwa bidi na maarifa yetu yote.

Usiogope kukosolewa: Kuna mtu aliyewahi kupata donda kwa kuchekwa au kusemwa? Kuna viumbe duniani vimekuja kukosoa tu, wao huwa hawana zuri wala baya … kwenye uandishi kukosolewa kunampandisha daraja mwandishi.

Hakuna kitabu hata kimoja duniani ambacho hakijawahi kukosolewa, watu wanakosoa vitabu vitakatifu sembuse muswada wako? Mimi kuna wakati natoa fedha kuwapa wahariri wakosoe kazi zangu! Ili iweje? Ili niwalishe watu chakula kizuri cha maandishi. Wanaokukosoa wanaweza kuwa watu wako wa karibu zaidi, tena wakakucheka kwa dharau lakini haimaanishi kwamba ulichoandika hakina maana.

Kuna watu wanaokusukuma ili uanguke lakini ukifanikiwa kusimama watakwambia walikusukuma ili usonge mbele… wapo wengi sana wanaokukosoa ili ushindwe lakini ukifanikiwa watajisifu wao ndio walihusika! Chukua hiyo leo.

Zingatia watu wa kuwaomba ushauri: Unapoamua kuwa mwandishi wa vitabu lazima uzingatie watu wa kuwaomba ushauri, unaweza kuharibu ndoto za maisha yako yote hapa duniani kwa kauli ya mtu mmoja tu. Sio kila mwenye mvi ana busara na maarifa hata wendawazimu wanazeeka eti!

Zingatia kuwa karibu na kuomba ushauri kwa wale watu wanaoendana na kazi zako. Wewe ni mwandishi wa riwaya, ukienda kuomba ushauri kwa mkemia asiyeamini kuhusu masuala ya vitabu vya kiswahili lazima atakukatisha tamaa.

Pia nawe muombe ushauri lazima uwe msikivu, mwenye mbinu na ndimi nzuri kwani watu wanaanza kukutazama kwanza kabla ya kukupa ushauri. Nusu ya uzuri wa binadamu upo kwenye ulimi wake. Jiangalie unazungumzaje na watu.

Usipende kujifananisha na waliokutangulia:  Ili uwe mwandishi mzuri lazima usome zaidi maandiko ya waandishi waliokutangulia.

Hakuna jambo jipya ambalo unaweza ukaandika leo likawa halijawahi kuandikwa na mtu yeyote duniani; Naweza kuwa mfuasi mzuri wa Shabani Robert lakini haimaanishi maandiko yangu yafanane na Shaban.

Kazi za fasihi ni za kibunifu, dhamira moja ya mapenzi inaweza kujadiliwa tofauti na waandishi hata mia moja. Maana yangu hapa ni kwamba lazima uwe mbunifu ili na watakaokuja wakusome wewe na sio marudio ya mtu mwingine.

Mwisho kabisa napenda niseme jambo kwa vijana wenzangu. Nchi hii sasa ni kubwa, ina watu zaidi ya milioni sitini. Vijana lazima tuwe wabunifu na wenye msaada kwenye nchi yetu, tuwasaidie viongozi wetu mawazo.

Tulitumikie taifa letu na ndio sifa pekee ambayo utajivunia uzeeni. Serikali najua mnanisikia, waandishi vijana na makini wapo, wenye kuibua fikra chanya kwenye jamii. Waandishi ni migodi ya fikra itumieni. Sisi tupo kwa ajili ya kutumika, tutumieni.

Umahiri wa ndege si kwa mbawa zake ndefu, ndivyo ilivyo pia kwa kijana umahiri wa kijana si kwa kujipamba kwake na kujipodoa bali ni bongo zake.

Tusichezee ujana wetu.  kijana mwenye kuchezea ujana wake atakuwa amepoteza siku zake za kupanda na mwenye kupoteza siku zake za kupanda lazima atazijutia siku zake za mavuno.

Pia duniani hatujaja na kitu na hatuwezi kuondoka na kitu, hii ni kweli kabisa lakini kwa mwandishi ni tofauti kidogo, sisi waandishi tukifa tunaacha akili zetu duniani. Tutaishi vizazi na vizazi, tuandikeni! Tuandikeni! Tuandikeni kama tunataka kuishi baada ya kufa.

Makala haya yameandaliwa na Ismail Himu mwandishi wa vitabu vya fasihi nchini Tanzania.

+255712631303/ +255736348

MITANDAO YA KIJAMII: AUTHOR ISMAIL HIMU

Author: Gadi Solomon