BURIANI MZEE HEGA

Habari za kushitua, machozi zinanimwaga
Zakupasua kifua, zimeshanijaza woga
Mola ameshachukua, roho ya Mzee Hega
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Alfajiri ya leo, aumwa tumesikia
Ghafla sasa kilio, mzee katangulia
Hili ni kubwa umio, nalo limetufikia
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Kauka bila kuuga, makubwa masikitiko
Mswahili mzee Hega, amefikwa na mauko
Mioyo inatupiga, kwa hili kubwa anguko
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Tumefiwa Waswahili, tumebakia twawaza
Mabaraza Kiswahili, BAKITA pia BAKIZA
Chozi njia mbili mbili, hakuna wa kunyamaza
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Wapenzi wa Kiswahili, pokea habari hiyo
Maradhi yamethakili, na leo kazima moyo
Akiwa Hindu Mandali, tumeangua kiliyo
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Laisa fii dunia, mzee ametutoka
Viongozi na raia, hatujui pakushika
Zahma imeingia, twabaki twatatarika
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Ya Rabi mola Kahari, mpe husuni hatima
Msahilishe safari, umpe makazi mema
Mtanulie kaburi, kwa upana na kwa wima
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Nyendo zako tutashika, Kiswahili washititi
Tutailinda hakika, lugha kwa kujidhatiti
Lugha ipate tanuka, ili yende na wakati
Buriani mzee Hega, pumzika kwa amani.

Dkt. Ahmad Sovu (PhD)
Malenga wa Ujiji-Kigoma
07 Aprili 2020

Author: Gadi Solomon