DUNIANI HATUNAYE, AMEONDOKA MARINI

Ai mama ai, haya makubwa majonzi
Sisi tulioko hai, zimetujaa simanzi
Taabani tuko mai, ametutoka kipenzi
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Ameondoka Marini, hivi sasa hatunaye
Marini bin Hassan, ndiye nimuhadithiye
Maisha ya duniani, ameyahajiri yeye
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Yamemfika mauko, Marini ameondoka
Ametangulia huko, jamii twasikitika
Makubwa masikitiko, nyuso zimesawijika
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Huu mzito msiba, poleni wanahabari
Mtangazaji habuba, TBC kahajiri
Pole Dkt. Rioba, kupoteza mmahiri
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Nakumbuka ufasaha, ukaapo mitamboni
Sauti yako ya raha, msikizi sikioni
Lakini leo twahaha, umeondoka machoni
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Kipindi cha ARIDHIO, ulikuwa ni mwanzishi
Ukakipa vivutio, kukipamba kwa nakishi
Umetwachia kilio, Sikitiko si ubishi
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Vipindi vya kuvutia, kwa kipajicho hakika
Sote tutakumbukia, cha KUTOKA AFRIKA
JAMBO ulitangazia, asubuhi ikifika
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

RAMADHANI ZANZIBA, ulikipa vidahizo
Kipindi kilichoshiba, kwa vionjo si mchezo
Tulikipenda sihaba, kwa vile vikorombwezo
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Safari hii ya haki, safari nenda salama
Hicho ndicho kilobaki, kuomba safari njema
Mwenyezi akubariki, akupe makazi mema
Duniani hatunaye, ameondoka Marini

Dkt. Ahmad Sovu (PhD)
Malenga wa Ujiji-Kigoma
02.04.2020

Author: Gadi Solomon