Huku Mwajaje?

1. Taratibu mlianza, kwa Mungu mliwezea,

Chekecheani mlika’, kabla moja kufika,

Pili mkafika, hesabu kuzihesabu,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

2. Nyepesi haikuwa, safari hii ndefu,

Mwakumbuka la saba? , mtihani wa taifa?

Sisahau ‘ne kidato, cha sita siulizi,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

3. Semista lianza, ya pili ikafuata,

Ya tatu hikukawia, ya nne hikuwa mbali,

Ya tano mchakachaka, sita na nane wengine,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

4. Digirii si haba, si sawia na vidato,

Lakini ni haba, si sawia na umahiri,

Si mwisho wa elimu, si mwisho wa safari,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

5. Sisahau wa vyeti, umahiri na zamili,

Ma’rifa hayo ni yetu, wala si yenu pekenu,

Huku nyumbani ni moto, twararua changamoto,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

6. Elimu mmeipata, tabu mta’ni situpe,

Twasubiri majawabu, ma’rifa yenu dhahabu,

Tupo twawangoja, sisite hata mmoja,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

7. Yapo mengi ya kueleza, wala hayaishi leo,

Tabu kubwa nisiwape, kusoma hi’ mishororo,

Masuluhisho mtupe, mfungue minyororo,

Hapo mmefika, huku mwajaje?

Amani Njoka, Swahili Hub

amanizacharyson@gmail.com

Author: Amani Njoka