Jipe moyo

Gadi Solomon, Swahili Hub
Naona mejinamia, tama umejishikia,
Kwa uchungu unalia, maisha kuyalilia,
Tamaa mejikatia, watamani kujifia,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Maisha ni kama njia, kila mtu tapitia,
Muhimu kupambania, lengolo kulifikia,
Ovyo uache kulia, aibu unajitia,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Safari bado ni ndefu, inuka funga mkanda,
Weka kando udhaifu, milima upate panda,
Utapata uzoefu, kufika unakokwenda,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Hata mbuyu lianza, kidogo kama mchicha,
Hilo wapaswa jifunza, ujaze lako pakacha,
Kamwe siruhusu funza, akilizo kupekecha,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Juani ukichumia, kivulini utalia,
Yafaa kulitambua, akilini kulitia,
Tabu unazopitia, mwisho zitakuinua,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Usiichoke safari, wala usirudi nyuma,
Mafanikio mazuri, kusumbukia lazima,
Haya uyatafakari, ukatende hima hima,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Beti saba naishia, moyo ndugu kukutia,
Penye nia pana njia, funzo ninakuachia,
Malengo kuyafikia, uanze kuweka nia,
Jipe moyo ndugu yangu, siku yako itafika.

Christopher Adelard
christopheradelard@gmail.com
0622588446/0763161191.

Hongera Rais
Chuo Kikuu Dodoma, shahada katunukiwa,
Ni shahada ya heshima, ya uzamivu twajuwa,
Wasifu waliusoma, tangu alipozaliwa,
Kongole kwake Rais, John Pombe Magufuli.

Pongezi nchi nzima, Magufuli katumiwa,
Kila mtu anasema, hakukosewa kupewa,
Busara zake hekima, na jopo ziliridhiwa,
Kongole kwake Rais, John Pombe Magufuli.

Mungu kampa karama, uwezo nao kapewa,
Akili hakumnyima, aweza kupambanuwa,
Ni neema za karima, na Allah amejaliwa,
Kongole kwake Rais, John Pombe Magufuli.

Ni haki ya mtu mwema, kwa mema kutambuliwa,
Katu asirudi nyuma, matunda yashuhudiwa,
Dua zetu twazituma, Magufuli waombewa,
Kongole kwake Rais, John Pombe Magufuli.

Hapa mwisho kadi tama, kongole nishazitowa,
Namuomba Allahuma, azidi kuongokewa,
Utambue wote umma, Magu si wa kuchezewa,
Kongole kwake Rais, John Pombe Magufuli.
Mwinyi .A. Mwinyi
Dar es Salaam
0767175191

Author: Gadi Solomon