SOKOMOKO: Wasichana wala hela

1. WASICHANA ni wazuri, ukikuwa nazo pesa,

Shababi muwe tayari, kwepuka hii mikasa,

Mnatupandisha mori, hamuoni ni makosa,

Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.

2. Wasichana mumezidi, wanaume walalama,

Mwavunja hata ahadi, wanabaki kuwasema,

Haja yenu si akidi, moyoni mnatuchoma,

Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.

3. Wasichana fikiria, wavulana wajipanga,

Fulusi mwaangalia, mwafikiri ndio mwanga,

Akina dada tulia, maisha ni kujipanga,

Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.

4. Wasichana fahamuni, tabia ni ya maana,

Msianguke shimoni, hela ni kama laana,

Mkiweka fikirani, mtajipata mwasona,

Tumechoka nazo simu, kila wakati ni hela.

LIONEL ASENA

‘Malenga Kitongojini’

Seeds High School, Kitale

Author: Gadi Solomon