TUJIKINGE NA CORONA: HOFU TUIPUKE

  1. Na tuiondoe hofu
    Kwa kujiweka nadhifu
    hatutapata harufu
    Virusi vyake Corona

2. Tuongeze wadilifu
Tuachane danganyifu
Serikaliye tukufu
Tuitegee sikio

3. Tuwe wana watiifu
Tuache tiana hofu
Baba Magu kaarifu
Kanuni zizingatiwe

4. Uzushi ni uhalifu
Wenye nyingi sumbufu
Siyo jambo kubalifu
Ameonya Majaliwa

5.Tuwe macho angalifu
Tandaoni kudurufu
Tusifanye haribifu
Corona kuupotosha

6.Ufundi wa kusarifu
Maneno nyambulifu
Tuyanyooshe sufufu
Kuelimisha Corona

7.Muumba wetu Raufu
Twakuomba na kusifu
Kwa dua zilonyoofu
Tuepushe na Corona

8. Mashee na Masharifu
Mapadri na Maskofu
Dua kwake Mtukufu
Kinga yake kwa Corona

9. Mikusanyiko nyunyufu
Mikono kuwa michafu
Ndio mambo karibifu
Corona kuambukiza

10.Tusiukate mkufu
Shambuliwe ja siafu
Kwani ndio turufu
Corona kuangamiza

Mtunzi: Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Author: Gadi Solomon