TUKIENZI KISWAHILI

Bismillahi awali,
Namshukuru jalali,
Aliyewezesha hili,
Mpaka likatimia.


Assalaamu alaykumu,
Enyi jamii kaumu,
Nyote mulofika humu,
Salamu nawatolea.

Ndugu nawasalimia,
Salamu nawatolea,
Kiswahili nimejia,
Kuja kuwaelezea.

Nina mengi ya kusema,
Kuyafikisha kwa umma,
Yarabbi nipe uzima,
Na nguvu nipate sema.

Mulojumuika hapa,
Jambo moja nitawapa,
Ni lugha iso na pupa,
Namaanisha hakika.

Naomba munisikize,
Yangu haya musibeze,
Kikosea siyalaze,
Kwani sijakamilika.

Umakini muchukue,
Akilini muyatie,
siogope munambie,
Pale ninapokosea.

Tukienzi kiswahili,
Ni muhimu Jambo hili,
Faida yake kamili,
Hakuna asotambua.

Kwani ndio ngao yetu,
Kuilinda lugha yetu,
Sie na vizazi vyetu,
Waje nao kuijua.

Nani asoifahamu,
Lugha yenye ukarimu,
Wanajifunza kwa hamu,
Kwa wale wasoijua.

Kuihusu lugha yetu,
Sie na jirani zetu,
Hilo twajivuna kwetu,
Kwa wao wageni wetu.

Vikaoni yatumika,
Lugha yetu msifika,
Uamuzi ulofika,
Twamshujuru rabuka.

Lugha hii muadhama,
SADC imeshazama,
Itumike bila hima,
Hilo limepita jama.

Kuna wale waloomba,
Na wakasema ya kwamba,
Wataka chukua namba,
Lugha hii kuisoma.

Twafurahi kweli kweli,
Lugha ilivyo nawiri,
Inasogea kikweli,
Tuifundishe kwa ari.

Wasomi oneni hili,
Tushughulike sanjari,
Tukienzi kiswahili,
Na wake utamaduni.

Hapa ninamalizia,
Siwachoshe waswahili,
Nia nishatimizia,
Kueleza jambo hili.

Mada niliyowambia,
Mola ifikishe mbali,
Tukienzi kiswahili,
Na wake utamaduni.

MTUNZI:IBRAHIM SULTAN RUBEIYYAH (Mshairi mpole)
ZANZIBAR,TANZANIA
0717089505
0715160597

Author: Gadi Solomon