Tutawakumbatia

Amani Njoka, Swahili Hub

1. Walimea meremeta, wakaishi humu,

    Kwa maji na chakula, tukatamani wadumu,

    Tukawakumbatia, nasi wakakaa.

2. Walitoka kwenda, simba na dubu kuwinda,

    Walienda kwa makundi, ni nani hakurudi?

    Tukawakumbatia, nasi wakakaa.

3. Tuliwatuma tena, hawakuchoka tena,

    Tulikuwa wana wao, ndiyo! wa kwao wana,

    Tukawakumbatia, nasi wakakaa.

 4. Kamwe hawakuchoka, kwao kupapigania,

    Walijipa ujiba, ubaba walijitwika,

    Tukawakumbatia, nasi wakakaa.

5. Hawa wetu wapenzi, kwa nyimbo na tenzi,

    Kuwalaki waliporudi, kwa vyote vipindi,

    Tukawakumbatia, nasi wakakaa.

6. Watamani niwataje, kitokwa machozi je?

    Wapo wapi niulize, wametuachia nani?

    Tukawakumbatia, nasi wakakaa.

7. Sasa twatawanyika, kwetu sio petu,

    Kwa nyundo na sepetu, twapuyanga peku,

    Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

8. Mtaa ni wetu, kila mahali ni kwetu,

    Wapi hasa ni kwetu? Mbona hatuoni katu?

    Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

9. Tumebaki twaranda, twasubiri parapanda,

    Hakuna tena msaada, tupo twatazama muda,

    Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

10. Twapewa majina, kwamba tu wa huku,

      Hakuna huruma, mtaani kunauma,

      Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

11. Wazazi wetu kututoka, wala hatukutaka,

      Ni nyakati zilifika, tukakosa furukuta,

      Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

12. Hii ni yetu barua, tafadhali sijeirarua,

      Uje kutuona huku, tunaishi kama kuku,

      Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

13. Mtaa hauna watoto, kuusingizia muache,

      Tumetoka kwenu humo, tafadhali msituache,

      Tuliwakumbatia, kwetu wakatoka.

14. Mwakwepa majukumu, kutwa kutuhukumu,

      Sisi sio sumu, kutupigia baragumu,

      Tutawakumbatia, msije mkatoka.

15. Kilio chetu kimefika, msingoje masika,

      Tutaja taabika, kwa zenu hulka,

      Tutawakumbatia, msije mkatoka.

amanizacharyson@gmail.com

0672395558

Author: Gadi Solomon