Maelezo ya utangulizi kuhusu Mashairi

Lugha ya Kiswahili ina tanzu zake za Kifasihi hususan katika usimulizi. Utanzu mkongwe kuliko zingine ni ushairi. Ushairi ulikuwapo  karne nyingi kabla ya ujio wa wageni kuja pwani ya Afrika Mashariki. Kwa mfano tungo za Fumo Luyongo ni miongoni mwa ushauri wa zamani katika upwa wa Afrika Mashariki kabla ya kuja kwa Waarabu.

Waswahili walijulikana  kwa majina ya jamii zao za asili za kibantu kama vile Walamu, Wapate, Wapemba, Wadigo, Wavumba, Waunguja, Wangazija, Watumbatu nk. Kihistoria tungo za fasihi ya Kiswahili hususan ushairi zilihifadhiwa katika hati ya Kiarabu.  Utanzu wa ushairi una historia ndefu miongoni mwa tanzu zote za kifasihi. E. Kezilahabi (Fasihi 111 1983) amegawa historia ya ushairi katika mihula minne ya Muhula wa Urasimu, Muhula wa Utasa, Muhula  wa Urasimu Mpya, Muhula wa Sasa.

Kimaandishi mashairi ya zamani yaliyojulikana sana  ni Utenzi wa Tambuka (1728) ulioandikwa na Bwana Mwego, Utenzi wa Hamziya (1690) ulioandikwa na Abdarus, Utenzi wa Al-Inkishafi (1810-1820) ulioandikwa na Sayyid Abdallah A. Nassir na Utenzi wa Mwanakupona  ulioandikwa na Mwanakupona mwenyewe. Kimaandishi Utenzi wa Al-Inkishafi ni utenzi wa kwanza wenye kujadili matatizo na mazingira ya Afrika Mashariki.  Utenzi wa Haziya unatumia lugha ya zamani na lugha iliyotumika ni ya Kingozi.

Utenzi wa Fumo Liyongo ni utenzi wa Ayubu, tenzi nyingine ni Utenzi wa Ngamia na Paa, Utenzi wa Masahibu, Utenzi wa Kayama, Utenzi wa Mikidadi na Mayasa, Utenzi wa Ras Al-Ghuli na Utenzi wa Shufaka, nk. Hizi ni tenzi za zamani na hazisomeki sana siku hizi.

Muhula wa Urasimu Mpya

Miaka ya 1945-1960 ni Muhula wa urasimu mpya. Huu ulikuwa ni wakati wa kina Shaaban Robert, Amri Abeid, Khamis Amani (Nyamaume), Mathias Mnyampala, Ahmed Nassir, Mdanzi  Hamasa, Kibwana Abdi Matunga, M.M. Kihere na wengine.

Kitabu cha Sheria za Kutunga Mashari kinahitajika sana. Muundo ulioshikana ni ule wa mizani 16 na mistari minne. Muundo huu ulitumiwa sana na Muyaka bin Hajj katika karne ya 18.

Mwaka 1960 – 67 ulikuwa ni muda wa kuyumbayumba  katika shairi wa Kiswahili. Hii ilisababishwa na nchi za Afrika Mashariki kutokuwa na malengo maalumu baada ya kupata uhuru.

Muhula wa sasa

Miaka ya 1967 hadi sasa washairi wengi walianza kuwa na mtazamo mpya wa kisanaa na mgogoro ulitokea wa uhuru wa kiuchumi, kiutamaduni na kadhalika . Suala la uhuru katika ushairi linafuata mkondo huu wa upya wa uakinifu wa kihistoria.

Ushairi wa Kiswahili uliathirika na:

  1. Kipindi kabla ya ujio wa wageni
  2. Kipindi kabla ya ujio wa Waarabu
  3. Wakati wa uvamizi wa Wareno
  4. Wakati wa Utawala wa Waoman
  5. Wakati wa Ujio wa Wazungu
  6. Baada ya Uhuru

Mgogoro uliibuka kutoka kwa wasomi walioanza kupinga muundo wa mashairi wa mapokeo na kuanza kutunga mashairi yasiyokuwa na muudo kamili. Wako waliouita mashairi ya mapingiti. Mgogoro huu wa mapokeo na wa kisasa unaendelea.

Author: Gadi Solomon