WAZIRI MWENYE DHAMANA

Nimezama baharini, bado sijafika mwaka
Lakini nimebaini, kunayo mengi mashaka
Naona tupo pembeni, sioni kufaidika
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Washairi mapokeo, kwa kweli twadhalilika
Na wale wa mamboleo, ndiyo wanaosifika
Mitandao na video, kote huko waoneka
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Mashairi yetu sisi, yamekuwa burudisho
Yani kwa lugha nyepesi, yamekuwa vichekesho
Malipo yetu msosi, tufanyapo maonyesho
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Nini kinashindikana, baba kutupa furusa
Tukawa twaonekana, nasi tukapata pesa
Naeleza kwa bayana, washairi tumenasa
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Nasi tupandishe chati, waziri mwenye dhamana
Tukuze misamiati, kila njia kila kona
Tuvae buti na suti, pale tunapokutana
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Maombi yangu sikia, najua yatakufika
Nafasi ngetupatia, mashairi kusikika
Radio runinga pia, mitandao kadhalika
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Tena iwe kila siku, isiwe kwa wiki moja
Mchana hata usiku, tusikilizwe pamoja
Mboso pale mimi huku, tutadumisha umoja
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Kalamu naweka chini, tamati natamatika
Leo hapa kituoni, lingine nitaandika
Ninaomba samahani, pale ulipokwazika
Waziri mwenye dhamana, washairi tukumbuke

Mtunzi:Sefu Makanyila
Lakabu:Moyo kichaka
Mahali:Jaribu Mpakani-Kibiti 🇹🇿
Mawasiliano:+255787141414

Author: Gadi Solomon