Afrika Kusini kuanza na shule 90 kufundisha Kiswahili

Amani Njoka, Swahili Hub

Johannesburg. Kuanzia mwaka 2020 Afrika Kusini itaanza kufundisha rasmi lugha ya Kiswahili kama lugha mbadala katika shule mbalimbali nchini humo kwa kuanza na shule 90.

Kiswahili itakuwa ni lugha ya kwanza kutoka nje ya Afrika Kusini kufundishwa katika shule za nchi hiyo ambayo tayari inakitumia kama Kifaransa, Kijerumani na Kimandarini zinafundishwa kama lugha za kigeni.

Miezi michache iliyopita Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imeridhia Kiswahili kuwa lugha yake ya 4, miongoni mwa lugha nyingine zinazotumiwa na jumuiya hiyo. Kiswahili kinatumiwa na SADC baada ya Kiingereza, Kireno na Kifaransa.

Kiswahili ndiyo lugha yenye asili ya Afrika inayozungumzwa na watu wengi zaidi duniani ikiwa na zaidi ya wazungumzaji 100 na sasa inavuka mipaka ya Afrika Mashariki. SADC wameanza kuitumia kama lugha ya mazungumzo kabla ya kuitumia katika nyaraka zake rasmi huku kikiwa lugha rasmi ya Umoja wa Nchi za Afrika tangu 2004 baada ya kupigiwa chapuo na mwenyekiti wa AU huo, rais mstaafu wa Msumbiji, Ndugu Joachim Chisano.

Lugha ya Kiswahili imepata umaarufu zaidi nchini Afrka Kusini katika siku za hivi karibuni bhaada ya msanii wa nchini humo, Maya Wengerf maarufu kama Sho Madjozi anayechanganya mashairi yake kwa Kiswahili. Wimbo wake wa hivi karibuni ‘Huku’ umepata umaarufu nchini humo ukiwa na watazamaji zaidi ya milioni 6 mtandaoni. Kuna uwezekano mkubwa wimbo huo ukampatia tuzo ya msanii bora wa kike kutoka B.E.T.

Gazeti la Daily National linaeleza kuwa msanii huyo anayeimba mziki aina ya ‘gqom’ alisoma katika jiji la Dar es Salaam ambako baba yake alikuwa akifanya kazi ingawa alizaliwa mjini Durban. Hata hivyo, Madzoji so msanii pekee kutoka nchini humo kuimba Kiswahili kwani mwanamuziki Miriam Makeba aliwahi kuimba nyimbo za Kiswahili zikiwamo ‘Hapo Zamani’ na ‘Malaika’

Mpaka sasa Kiswahili kinazungumzwa katika nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na sehemu za Msumbiji, Somalia, Visiwa vya Komoro, sehemu za kaskazini mwa Zambia na Malawi pamoja na sehemu nyingine kuunda idadi ya wazungumzaji zaidi milioni 150 ulimwenguni.

Tayari Kiswahili ni lugha rasmi katika ukanda wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki huku Rwanda ikiifanya lugha ya taifa tangu mwaka 2017 baada ya Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza.

Vilevile serikali ya Uganda imedhamiria kuanzisha baraza la Kiswahili la Taifa kwa kushirikiana na Kamisheni ya Kiswahilin Afrika Mashariki ili kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya pili baada ya Kiingereza

Author: Amani Njoka