Buriani Mzee Maina

Ikiwa ni wiki chache tangu kuondokewa na mwanzilishi wa Swahili Hub Profesa Ken Waribora, kwa mara nyingi tasnia na uga wa Kiswahili umekumbwa na simanzi baada ya kumpoteza nguli na miongoni mwa waanzilishi wa Swahili Hub, Mzee Stephen Maina.

Kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, Theresia Paul, nguli huyo wa Kiswahili aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) alifariki kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kisukari kwa muda mrefu. Mzee Maina alifariki nyumbani kwake, Ubungo Maziwa, jijini Dar es Salaam akiwa na familia yake.

Mkewe alieleza kuwa, marehemu Mzee Maina alianza kuzidiwa tangu tarehe 24, Aprili 2020 ambako aliwahishwa Hospitali ya Regency kupatiwa matibabu baada ya sukari kushuka ghafla. Baada ya juhudi madaktari aliruhusiwa kurejea ambapo familia iliendelea kumhudumia mpaka Jumamosi, tarehe 2, Mei 2020 alipozidiwa tena na mauti kumkuta nyumbani kwake.

Taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi zinafanyika nyumbani kwake, Ubungo Maziwa. Ibada ya kuaga mwili wa marehemu itakayofanyika Jumanne, tarehe 5, Mei 2020 katika Kanisa Katoliki Makuburi, jijini Dar es Salaam.

Author: Amani Njoka