Chaukidu yaandaa kongamano la Kiswahili

Kifupi: Katika miaka 100 tangu kuanza kwa shughuli za usanifishaji wa Kiswahili kumeendelea kuwa na mijadala mingi juu ya utumizi wa Kiswahili Sanifu na vijilugha vingine vya Kiswahili, katika maeneo tofauti hasa Afrika Mashariki na hivyo kuchochea utafiti zaidi.

Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (Chaukidu) wameandaa kongamano litakalowakunanisha wataaluma, watafiti, wanafunzi na wadau wa Kiswahili litakalofanyika Mombasa nchini Kenya.

Kongamano hilo limepangwa kufanyika kwa siku mbili, tarehe 15-17 mwezi Decemba, 2020 katika Chuo Kikuu cha Pwani, mjini Kilifi. Kongamano hilo litawakutanisha wakereketwa wa lugha ya Kiswahili pamoja na wanataaluma mbalimbali duniani kwa ajili ya mustakabali wa lugha hiyo tangu usanifishaji wake.

Taarifa iliyotolewa na Chaukidu inaeleza kuwa, kutakuwa na mada mbalimbali zitakazochokoza mijadala katika muendelezo wa mijadala lukuki kuhusu hatma na mustakabali wa Kiswahili duniani huku mada kuu ikiwa ni: Kiswahili na Viswahili: Kuelekea Karne Moja ya Usanifishaji.

Mada itakitwa katika tafiti zitakazojadili mchango na changamoto ya usanifishaji wa Kiswahili katika mawanda tofautitofauti kama vile; Isimujamii, Tafsiri na Ukalimani, Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) , Uandishi wa habari na utangazaji na Uchapishaji katika Kiswahili .

Mawanda mengine ni; Ufundishaji wa Kiswahili shuleni na vyuoni , Ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, Kiswahili na Siasa (ushirikiano, utawala bora, demokrasia na maendeleo) , Filamu, futuhi, na vibonzo • Muziki (bongofleva, taarabu, injili, nk) , Kiswahili na lugha ya/za kufundishia , Kiswahili na Lugha za jamii ndogondogo.

Hizo ni baadhi tu ya mada mbalimbali ambazo zitajadiliwa katika kongamano hilo ambalo litatoa picha ya hali ya Kiswahili Sanifu tangu kusanifishwa kwake mpaka hivi leo.

Ungana na Swahili Hub ka habari za moja kwa moja kutoka Chuo Kikuu cha Pwani kwa ajili ya habari zihusuzo kongamano hilo kuanzia siku ya kwanza mpaka mwisho.

Author: Amani Njoka