Chaukidu yaungana na wapenzi wa Kiswahili kumlilia Profesa Ken Waribora

Gadi Solomon, Swahili Hub

Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu) kimeungana na Wakenya, wapenzi wa Kiswahili duniani kote pamoja na vyama mbalimbali vya Kiswahili na Fasihi kuombolezea msiba wa Profesa Ken Walibora aliyefariki kwa ajali juzi Jumatano.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Rais wa Chaukidu, Profesa Leonard Muaka, imeeleza kwamba Prof. Ken Walibora alikuwa Rais wa kwanza wa CHAUKIDU na jumuiya ya wanachaukidu imesikitishwa sana na kifo chake.

Alisema kupitia taarifa hiyo kuwa “Ni vigumu sana kumwelezea Prof. Walibora kwa lugha ya kawaida pasipo kuhafifisha makubwa ambayo ameifanyia jamii yake na wapenda Kiswahili kote duniani.”

“Wengi wanafikiri kwamba ni maandiko na amali zake tu katika mawanda ya fasihi na utangazaji yampayo heshima na utitiri wa waombolezaji kama tulivyoona tangu usiku wa Jumanne tetesi za kifo chake zilipoanza kusambaa. La hasha! Ken Walibora alikuwa zaidi ya mwandishi, na zaidi ya mtangazaji,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Chaukidu ni Chama cha Waswahili wa dunia nzima, kikijumuisha Waswahili wote waishio Afrika Mashariki na wale waishio katika diaspora, au ughaibuni, kama wengi wapendavyo kuiita. Vuguvugu lililopelekea uanzishwaji wa chama hiki lilianzia ughaibuni, nchini Marekani miaka ya 2000.

Chama kilipoundwa rasmi mwaka 2011 na hatimaye kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza mwaka 2012, marehemu Ken alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa chama hiki  ambacho kimekuwa chama kikubwa zaidi na kiungo muhimu kwa wadau na wapenzi wa Kiswahili nyumbani na ughaibuni. Hata baada ya urais, ndugu Ken aliendelea kuwa mjumbe wa bodi ya Chaukidu kwa miaka yote mpaka mauti yalipomvamia bila huruma. 

Bodi ya awamu ya pili ya Chaukidu ilipoamua kupeleka makongamano ya kimataifa ya Chaukidu Afrika Mashariki, Prof. Ken alikuwa mstari wa mbele kulipigia debe kongamano hilo, ambalo lilifanyika mwaka 2016 katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, jijini Nairobi, akishirikiana na wadau wengine.

Marehemu Prof. Walibora ni mwanazuoni wa kupigiwa mfano. Waswahili kwa ujumla wamepoteza askari na jemadari mahiri katika mawanda ya habari, utangazaji, uandishi, utafiti, utetezi wa Kiswahili, na ufundishaji wa lugha na fasihi ya Kiswahili.

Author: Gadi Solomon