Chawakita-MUM wamkumbuka Shaaban Robert

Na Dk Ahmad Sovu

Kifupi: Chuo Kikuu cha Kiislamu cha mkoani Morogoro (MUM), Jumatano (1/1/2020) kiliandaa kongamano maalumu kwa ajili ya kumuenzi mwanafasihi mashuhuri Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, Shaaban Robert.

Katika kongamano hilo, washiriki walihimizwa kukitumia Kiswahili ipasavyo kama sehemu ya kumuenzi nguli huyo wa mashairi pamoja na kupata fursa mbalimbali.

Morogoro. Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Vyuo Vikuu vya Tanzania (CHAWAKITA) Tawi la MUM wameadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa baba wa Fasihi ya Kiswahili Shaaban Robert huko Morogoro Tanzania Siku ya Mwaka mpya 2020.

Mgeni Kiongozi katika hafla hiyo alikuwa Karii na mshairi maarufu Ustadh Mzee Sudi Ameir Andanenga. Mzee Andanenga aliambatana na watoto wawili wa marehemu Kaluta Amri Abeid ambao ni Sheikh Barki Kaluta na Ameir Kaluta.

Mgeni Kiongozi, Ustadh Andanenga maarufu kama sauti ya kiza kwa lakabu ya kishairi kuwa alikuwa ni mtu wa aina yake katika lugha ya Kiswahili kwa fasaha na tungo.

“Marehemu Shaaban Robert tulikuwa tukionana sana, hasa anapokuja Dar es Salaam, maeneo ya Kariakoo kwa bwana mmoja wa Tanga. Ulikuwa ukikaa naye humwishi,” alidadavua Andanenga.

Naye Mtiva wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za jamii, Dk Salim akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo alisema, vijana wajitahidi kutumia Kiswahili kwa ufasaha kama wanavyofanya kina Andanenga.

Mwenyekiti wa CHAWAKITA Taifa, Vitoni Pamagila alisema pamoja na kuadhimisha Siku ya Shaaban Robert, pia amewakumbusha wanachama kujisajili katika kanzidata ya chama kwa ajili ya kupata idadi kamili ya wanachama.

Katika hatua nyingine baadhi ya wanafunzi wameshinda tuzo za mshairi bora. Walioshinda ni wanaume wawili na mwanamama mmoja.

Akitoa salamu zake, Mshtiti Dkt. Ahmad Sovu kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, amewataka vijana kusoma na kuijua historia ya Shaaban Robert na kuwataka wana MUM kukithamini na kukipenda Kiswahili kwa kuwa kina manufaa mbele.

Sheikh Bark Kaluta na Nduguye Ameir wamewasisitiza vijana kuishi kwa kumcha Mungu kama kina Andanenga, Shaaban Robert, Mathias Mnyampala na Kaluta Amri Abeid kwani wao waliishi kichamungu na hata mashairi yao yalijaa ujaala.

Maadhimisho hayo yaliambatana na michezo ya mpira wa pete, miguu, kukuna nazi, bao n.k. Mlezi wa CHAWAKITA, Abdallah Hamad pamoja na Mkuu wa Idara ya Kiswahili chuoni hapo, Dk Nawaje Mganga wamewashukuru wadau wote waliohudhuria wakiwamo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mzumbe, Rucu na Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere.

Kongamano hilo lilikuwa na kaulimbiu ‘Kiswahili Chetu, Urithi Wetu’ na mada kadhaa za ushairi, hadithi fupi, utenzi na vitushi ziliwasilishwa.

Author: Amani Njoka