Chuo Kikuu Huria chang’ara Kongamano la Kimataifa la Kiswahili Zanzibar

Na Dkt. Mohamed Omary Maguo

Zanzibar. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepata heshima kubwa katika Kongamano la Kimataifa la Kiswahili linalofanyika hapa Zanzibar kuanzia leo 19-20/12/2019 na kuhusisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Chuo kimepata heshima baada ya kukabidhi tasinifu zaidi ya 60 za wahitimu wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Kwa Mgeni rasmi Mhe. Balozi Seif Ali Idi Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar. Wahitimu hawa ni kutoka Pemba tu.

Tasinifu hizi zilizokabidhiwa kwa mgeni rasmi ni sehemu tu ya wahitimu wa shahada ya Uzamili ya Kiswahili zaidi ya 150 waliohitimu tangu Programu ilipoanza miaka 6 iliyopita. Idadi ya wahitimu kutoka OUT kwa Programu hii ni kubwa mara dufu ya wahitimu wa UDSM, SUZA na UDOM. Hili limetajwa bayana katika hotuba ya Mgeni rasmi.

Wahitimu watatu wa Shahada ya Uzamivu wa OUT ambao ni Wanzibari pia wamepata fursa ya kukabidhi tasinifu zao na kushikana mkono na Mgeni Rasmi. Wahitimu ni Dkt. Adam Omar, Dkt. Haji Makame Ussi na Dkt. Maimuna Makalo.

Tunawapongeza sana kwani kupitia kwao Chuo kimeendelea kufahamika na kuheshimika. Pia, baadhi ya wanakongamano wameona kuwa inawezekana kusoma Uzamivu OUT na kufanikiwa.

Kuwepo kwa walimu watatu wa Idara ya Lugha na Isimu ya OUT kuwasilisha mada mbalimbali katika Kongamano hilo pia ilikuwa ni heshima kubwa kwa Chuo Huria.

Walimu hao ni Dkt. Mohamed Maguo, Dkt. Salma Hamadi na Mwl. Bakari Kombo. Kwa Hakika OUT imesikika na inaendelea kisikika na kung’ara zaidi kitaifa na kimataifa.

Author: Amani Njoka