IDEA AFRICA waanzisha kampeni za kukipaisha Kiswahili Umoja Mataifa

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Shirika la Idea Africa kupitia wavuti yake ya change.org imeanzisha kampeni maalum ya kutafuta sahihi takribani 1000 kama njia pekee ya kulishinikiza baraza la Umoja wa Mataifa kukitumia Kiswahili katika shughuli zake rasmi.

San Francisco. Kufuatia hatua kadha wa kadha za Kiswahili kukuzwa na kuenezwa kwa kasi kubwa kuendelea kuchukuliwa, wavuti ya Change.Org imeanzisha kampeni maalum ya kukusanya saini za nyingi kadri iwezekanavyo ili Kiswahili kipewe hadhi ya kuwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Umoja wa Mataifa.

Sababu ya shirika hilo kufanya hivyo ni baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwa, kambi kubwa za wakimbizi Afrika zote ziko kwenye eneo la Afrika Mashariki (kambi 10 kubwa zaidi) na ni ukanda ambao wazungumzaji wake wengi hukitumia Kiswahili kama lugha rasmi. Wanajamii na wanaojitolea kusaidiana kwenye kambi huzungumza Kiswahili na kufunzwa na Kiswahili pia. Waafrika wengi maeneo mengine wameanza kukumbatia Kiswahili.

Kitendo cha serikali ya Afrika Kusini kutangaza kuanza kukitumia Kiswahili katika shule za msingi 2020, imekuwa ni ishara kuwa Kiswahili ni lugha ambayo inakumbatiwa Kiafrika na hivi karibuni itakuwa lugha ambayo mataifa mengi ya Kiafrika yatazingatia.

Mpaka hivi sasa lugha kama Kifaransa, Kiarabu na Kihispania bado ni lugha inayopendelea katika matumizi mengi ya kazi katika mkoa wa Afrika Mashariki na Afrika kama bara kwa ujumla. Tungepends kiswahili kiongezewa kama kama sehemu ya hitaji kwa lugha za Umoja wa Mataifa. Itasaidia katika kungetengeneza miradi zaidi ya jamii inayohusika hasa ukizingatia kuwa tayari Kiswahili ni lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Nchi Huru za Afrika na SADC.

Mtandao huo uliendelea kueleza kuwa uwapo wa ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi kama makao makuu ya ofisi za Jumuiya hiyo barani Afrika sambamba na mashirika mengine, ilipaswa kuwa sababu inayotosha kufanya mapinduzi hayo kwani watu wanaohudumia na ofisi hizo wengi ni Waswahili.

Ikumbukwe kuwa mashirika ya Umoja huo kama Shirika la Mazingira (UNEP) na Shirika la makazi ya Wanadamu (UN-HABITAT) pia zina ofisi zao jijini Nairobi. Vilevile IFRC, Oxfam, CARE, ni kati ya mashirika mengine ya kimataifa ambayo yana ofisi katika maeneo ambayo yana wazungumzaji wengi wa Kiswahili kama Lugha ya taifa.

Kampeni hiyo yenye kaulimbiu ‘Make Swahili One of the UN Official Language’ (Kifanye Kiswahili kuwa moja ya Lugha Rasmi za Umoja wa Mataifa) inaendeshwa kupitia wavuti ya Change.Org na mpaka sasa imekusanya saini zaidi ya 500 ambazo zimekuwa zikisainiwa mtandaoni na wadau na wakereketwa wa lugha ya Kiswahili tangu miezi minne iliyopita.

IDEA AFRIKA ni shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake mjini San Fransisco nchini Marekani ambalo hujishughulisha na masuala ya kijamii kama vile wakimbizi, watoto wa mtaani na wanaoishi katika mazingira magumu pamoja unyanyasaji wa kijinsia.

Author: Amani Njoka