Italia waja na kongamano la Kiswahili na utamaduni

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Kongamano hilo litakawakutanisha watafiti, wadau na wanasayansi wa lugha na tamaduni mbalimbali kujadili kuhusu mustakabali wa lugha ya Kiswahili. Mada mbalimbali kuhusu lugha ya Kiswahili ikiwemo fasihi ya Kiswahili, Semantiki ya Kiswahili, ukuzaji wa mtaala wa Kiswahili, mbinu za ufundishaji Kiswahili na nyingine nyingi zitajadiliwa na washiriki.

Roma. Chuo cha Sayansi, Uhandisi na Teknolojia cha Mjini Roma, Italia kimeandaa Kongamano la Lugha ya Kiswahili na Utamaduni litakalofanyika kwa siku mbili tarehe 13-14 Desemba, 2021. Kongamano hilo litahudhuriwa na wasomi na watafiti mbalimbali wa lugha kutoka vyuo vikuu kadhaa ulimwenguni kutoka Marekani, Kanada, Japani, Australia, Nigeria, Uingereza na Falme za Kiarabu.

Kongamano hilo litawaleta pamoja wasomi na watafiti wa lugha ya lugha ya Kiswahili kujadili maendeleo na changamoto zinazoikabili lugha hiyo pamoja na kutafuta masuluhisho ya changamoto hizo. Vilevile wasomi hao watabadilishana uzoefu kuhusu Kiswahili na utamaduni wake kwa kusisitiza uwapo wa tafiti zaidi, uvumbuzi na mbinu mpya katika kuiimarisha lugha ya Kiswahili na Utamaduni.

Wasomi na watafiti hao watawasilisha mda mbalimbali ikiwemo fasihi ya Kiswahili, Semantiki ya Kiswahili, Pragmatiki ya Kiswahili, Ukuzaji wa mtaala wa Kiswahili, Mbinu za Ufundishaji wa Kiswahili, Upimaji wa lugha ya Kiswahili na mada nyinginezo. Kongamano hilo litakuwa ni la aina yake kwa kuwa ni kongamno kubwa zaidi kuwahi kuandaliwa na chuo hicho cha Sayansi, Uhandisi na Teknolojia.

Akizungumzia kongamano hilo, Mkurugenzi Mshiriki wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), Dk Mussa Hans alisema hiyo ni fursa Kiswahili kupanuka zaidi.

“Hii ni kati ya fursa muhimu na nzuri kwa lugha ya Kiswahili kuendelea kuzungumzwa sio tu nje ya mipaka ya Afrika ya Mashariki bali hata nje ya Afrika,” alisema Dk Hans.

Vilevile makala,vitabu na machapisho mbalimbali kuhusu lugha ya Kiswahili yatazinduliwa katika kongamano hilo na yatapatikana mtandaoni bila gharama yoyote. Hii ni ishara nzuri ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili kuendelea kushika hatamu ulimwenguni.

Hivi karibuni lugha ya Kiswahili imepata mashiko sehemu katika meneno mengi ulimwengu na ni wakati ambao Kiswahili kimekubalika zaidi kuliko wakati wowowte ule. Mpaka sasa Kiswahili kimepenya katika shughuli rasmi ikiwemo mikutano ya kimataifa kama ile ya AU na SADC.

Author: Gadi Solomon