Jumuiya ya Waswahili Marekani yabadilisha jina

Gadi Solomon, Swahili Hub

Dar es Salaam. Jumuiya ya wazungumzaji Kiswahili nchini Marekani imetangaza kuanzia sasa itatambulika kama Swahili Society America (SSA) wakiachana na jina la awali Swahili Society USA, huku wakibaki na malengo yaleyale ya awali katika mitandao ya kijamii, tovuti pamoja na shughuli zake kwa ujumla.

Taarifa iliyotolewa  juzi Jumanne na mmoja wa waanzilishi wa chama hicho, Mwenyekiti Liberatus Mwangombe, imeeleza kwamba jina la awali Swahili Society USA kuanzia sasa halitatumika, vilevile wamejipanga kwa shughuli mbalimbali kwa mwaka 2020.

Alisema mabadiliko hayo yanahusu jina la chama hicho, nembo  na mwonekano mpya pamoja.

Alisema lengo kuu la chama hicho ni kuwakutanisha pamoja wazungumzaji wa Kiswahili kwa kuangazia masuala ya kijamii, kiutamaduni na uchumi mambo yenye kuleta  maendeleo kwa jamii ya wazungumzaji wa Kiswahili.

Mwenyekiti Mwangombe alisema malengo mahususi ya chama hicho, ni kuimarisha mawasiliano baina ya jamii za wazungumzaji Kswahili nchini Marekani na  nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Pia, kukitangaza na kukiendeleza Kiswahili katika masuala ya kijamii katika jamii ya wazungumzaji Kiswahili,

Vilevile, kuhamasisha wanataaluma na kutafuta fursa, kuutangaza utamaduni wa Kiswahili, maarifa na ushirikiano wa kibiashara kwa wananchama kwa kushirikiana na serikali za nchi husika, mashirika na wafanyabiashara.

Author: Gadi Solomon