Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere chaandaa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili

Gadi Solomon, SwahiliHub

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere katika Taaluma za Kiswahili kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Uhuru Media Group, wameandaa Kongamano la Kimataifa la Kukumbuka mchango wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kukuza Kiswahili na harakati zake za Ukombozi.
Akizungumzia kuhusu maandalizi ya Kongamano hilo ofisini kwake, Mgoda Profesa Aldin Mutembei amesema maandalizi yanaendelea vizuri na watu kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki Kongamano hilo la siku mbili litakalofanyika Aprili 16 na 17 mwaka huu.
“Maandalizi yanaendelea na tunayo kamati ya maandalizi ambayo tunakutana mara moja kwa wiki ili kuweka mikakati na kupeana taarifa,” alisema Profesa Mutembei.
Mgoda huyo alisema Kongamano hilo litawajumuisha watu mbalimbali. Hivyo amewahimiza wajitokeze kwa wingi siku ya Kongamano kwenye Ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mada kuu kwenye Kongamano hilo itakuwa Lugha na Ukombozi: Nafasi ya Kiswahili katika kufanikisha Ukombozi na Uenezi wa Itikadi na utaifa wa umajumui barani Afrika.

Ukumbi wa Nkurumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao litafanyika Kongamano wa Kimataifa wa Kiswahili Aprili 16 na 17 mwaka huu.


Wasemaji wa Kongamano hilo wanatarajiwa kutoka Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Guinea Bissau, Namibia, Comoro na Afrika Kusini. Pia Kongamano hilo litawapa nafasi wapigania ukombozi katika nchi za Uganda, Rwanda na Sudan Kusini ambao walikaa Tanzania katika maandalizi ya kuleta ukombozi wa nchi zao. Washiriki hao watapata nafasi kueleza wanaikumbukaje lugha ya Kiswahili katika kuandaaa mikakati na hatimaye kufanikisha mipango yao ya ukombozi.
Lengo la Kongamano hilo ni kufufua ari ya Kiswahili kama lugha ya ukombozi ya Kiswahili katika itikadi na utaifa wa umajumui wa Kiafrika. Vilevile ni kutambua mchango wa vyama vya ukombozi katika kukidumisha na kukisambaza Kiswahili.
Mada zingine ndogondogo ni zitakuwa Kiswahili na Ukombozi kabla na wakati wa uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.
Nafasi ya lugha ya Kiswahili na Tanzania katika ukombozi wa nchi za Kiafrika.
Ujifunzaji na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika nchi za SADC, Nafasi ya Mwalimu Nyerere katika kuimarisha ukombozi.
Mchango wa Tanzania katika kufanikisha ukombozi, Lugha na ukombozi wa mwanamke barani Afrika. Lugha na ukombozi wa mwanamke barani Afrika, Lugha na elimu ya ukombozi, Lugha ya Kiswahili na ukombozi kiuchumi, Lugha ya Kiswahili na uendezo wa itikadi na utaifa wa umajumui wa Kiafrika.
Vilevile, lugha katika falsafa ya elimu ya kujitegemea, Lugha na ujenzi wa utu wa binadamu, Nafasi ya Kiswahili katika kuimarisha jeshi, Nafasi ya Kiswahili katika usalama na ulinzi, Fasihi ya Kiswahili na dhana ya ukombozi

Author: Gadi Solomon