Kiswahili kimeendelea kuwa mjadala Uganda

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Kiswahili kitafanyika msaada mkubwa hasa kwa wazungumza wanaotoka katika nasaba tofauti za lugha mama. Wazungumzaji kutoka lugha mbalimbali wanaweza kukutana na wakashindwa kuelewa lakini ikiwa Kiswahili kitapewa nafasi basi kinaweza kuwa daraja bora kwa watu kuelewana.

Kampala. Wakati hatua mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kukisukuma Kiswahili kuwa lugha itakayotumika katika nyanja zote nchini Uganda, kumeonekana kuwa na hofu kwamba huenda lugha za makabila zikafa. Hata hivyo, hoja hiyo imeonekana kuwa dhaifu kwa sababu tayari Kiswahili kimekuwa ni lugha rasmi katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki na lugha za makabila bado zinazungumzwa.

Daily Monitor liliandika, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Uganda Peoples Congress, Hayati Joseph Bossa aliwahi kusema kuwa hakuna haja ya kuwa na hofu kuhusu lugha ya Kiswahili kwa sababu kitarahisisha mawasiliano na mafunzo shuleni pia. “Hakuna haja ya kuwa na hofu kwamba Kiswahili kitazimeza lugha za makabila. Watu watakuwa huru kuzungumza na kuzitumia lugha zao za makabila miongoni mwao.” Pia aliongeza kuwa, kwa kipindi chote cha miaka 34 ambacho serikali ya Rais Museveni imekuwa madarakani, ulikuwa ni wakati muafaka kwa Kiswahili kuwa lugha ya taifa la Uganda kwa kutumiwa na raia na mwisho aliwahi kuhoji, “ni kipi ambacho kimezuia hilo kwa muda wote huo?”

“Wakati wa mapokezi na uzinduzi wa ndege mpya iliyonunuliwa na Shirika la Ndege la Uganda ambapo watu nilisikika wakitumia lugha mama ambayo ilikuwa vigumu kueleweka kwa walio wengi na hivyo kuonekana kuwa ni vyema nchi nzima ikajifunza Kiswahili ili iwe rahisi kwa watu wote kuweza kuelewana. Watu walikuwa wakisalimiana ‘abeyibo ladies and gentlemen” mwingine “tusanyuse okkulaba ladies ande gentlemen”, hii haitoshi, inapaswa tupate lugha ya kutuunganisha kama taifa.”

Gazeti la Daily Mirror siku ya Jumapili, tarehe 3 Novemba lilieleza namna Hayati Bossa alivyotamani lugha ya Kiswahili iwe lugha ambayo itatumika na jamii kwani italeta maelewano zaidi kuliko lugha mojamoja licha malalamiko kuwa Kiswahili kitazipoteza lugha mama pamoja na utamaduni wake.

Nchini Uganda watu mbalimbali wanaonekana kupata changamoto katika matumizi ya lugha ya Kiswahili hasa kwa kuwa sehemu mbalimbali kama benki, maduka makubwa na taasisi za elimu zinatumia Kiingereza kwa hiyo ita vigumu kwa watu kukielewa Kiswahili.

Lugha ya Kiswahili imekuwa daraja la mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji wa lugha nyingi za makabila katika nchi kama Tanzania ambayo ina makabila zaidi 120 lakini bado makabila hayo yanazungumza lugha zao. Kwa sasa lugha ya Kiswahili imeendelea kushika hatamu Afrika Mashariki, Afrika na Duniani.

Tayari Kiswahili kimekuwa rasmi katika jumuiya mbali za Afrika huku kikifundishwa katika mataifa mengi ulimwenguni. Uganda inaonekana kususua katika matumizi ya Kiswahili huku woga wa kupotea kwa lugha zake za asili kuwa miongoni mwa sababu kuu.

Author: Gadi Solomon