Masanja Mkandamizaji kusherehesha tamasha la Kiswahili Marekani

Amani Njoka-Swahili Hub

Kifupi: Tamasha hilo litakalofanyika Novemba mwaka huu linalenga kuwaleta pamoja jamii ya Waswahili wanaoishi Marekani na sehemu nyingine ulimwenguni. Itakuwa ni fursa nzuri kwa watu kufahamiana, kula pamoja na kuzungumza masuala mbalimbali yahusuyo maendeleo ya Kiswahili na utamaduni wake.

Maryland, Marekani. Chama cha Wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili waishio Marekani (Ssusa) katika Jimbo la Maryland kimeandaa tamasha la Kiswahili na Utamaduni ambalo litawakutanisha pamoja wazungumzaji wa lugha hiyo kutoka sehemu mbalimbali na maeneo ya jirani ya kama Philadelphia, Delaware, West Virginia na Northern Carolina ili kutangamana na kufahamiana zaidi.

Taarifa kutoka katika mtandao wa chama hicho inasema kwamba tamasha hilo litashereheshwa na msanii na mchekeshaji, Masanja Mkandamizaji (Tanzania). Tamasha hilo litafanyika Novemba 2, 2019 litawakutanisha Waswahili ikiwa ni pamoja na familia zao kwa ajili ya kuenzi utamaduni wa Waswahili.

Chama hicho ambacho kimejengwa katika misingi ya umoja, uhuru, amani na upendo hufanya matamasha hayo mara kwa mara yenye lengo la kuwainua na kuwasaidia watu wenye asili ya Afrika wanaozungumza Kiswahili kiuchumi na kijamii. Chama hicho hutoa msaada wa kuwainua kiuchumi watu mbalimbali wanaozungumza lugha ya Kiswahili katika nchi yote ya Marekani.

Hii ni fursa ya kipekee ya kujumuika na kutangamana pamoja kuienzi asili ya Waswahili na utamaduni wake kwani kutakuwa na ngoma, nyimbo na vyakula vyenye asili ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Tamasha la mwaka huu limepewa jina la Night Dinner and Dance Gala ni miongoni mwa matukio adimu kufanyika katika nchi za ughaibuni.

Author: Gadi Solomon

2 thoughts on “Masanja Mkandamizaji kusherehesha tamasha la Kiswahili Marekani

Comments are closed.