Mbunge ashauri Bunge kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili

Ahmad Sovu (PhD)

Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha kundi la Vijana, Zaynab Katimba amelishauri Bunge kuona haja ya kuanza kutunga sheria zake katika lugha ya Taifa lugha yetu ya Kiswahili.

Mbunge Katimba aliyasema maneno hayo jana bungeni alipokuwa akichangia muswada wa mabadiliko mbalimbali ya sheria.

“…Nadhani katika siku zinazofuata, kwa msingi uleule wa kuunganisha Watanzania kwa kutumia lugha ya Kiswahili, lakini basi kwa msingi uleule wa kukuza na kuendeleza lugha yetu ya Taifa ya Kiswahili ifike wakati basi hata hapa bungeni tuone haja ya kutunga sheria kwa kutumia lugha yetu ya Taifa lugha yetu ya Kiswahili…” alisema Katimba.

Katimba aliendelea kusema kuwa, kwa muda mrefu sheria nyingi hapa bungeni tunazitunga kwa kutumia lugha ya Kiingereza.

Maoni ya Katimba yamekuja katika wakati mwafaka, kwani katika awamu hii ya 5 inayoongozwa na Rais John Magufuli tumeshuhudia akitoa mchango mkubwa uliotukuka katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili.

Aidha, makala ya ( Sovu 2016) yaliyochapishwa katika jarida la Mulika la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anaeleza mchango wa Rais Magufuli katika maendeleo ya Kiswahili kuwa ni pamoja na, kuongeza fursa za ajira za Kiswahili, kukuza msamiati na misemo ya Kiswahili, kukuza taaluma ya tafsiri na ukalimani na kuondoa kasumba mbaya juu ya lugha ya Kiswahili na kadhalika.

Akifafanua bungeni hiyo jana, Katimba amesema msingi wa kukuza lugha ya Kiswahili uliasisiwa na Baba wa Taifa na umeendelea kuungwa mkono na kusimamiwa ipasavyo na Rais Magufuli kwa kuendelea kuwaunganisha Watanzania kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Katimba aliendelea kusisitiza kuwa, marekebisho hayo yatakuwa na tija sana kwa wale wasiokuwa na ufahamu mzuri wa lugha ya Kiingereza.

Kutokana na hayo, wataalamu mbalimbali na wapenzi wa Kiswahili wamempongeza Katimba kwa maoni yake hayo.

Wanasema imekuwa ni kilio kikubwa kwani wanapenda lugha ya Kiswahili ndio itumike katika kila shughuli za serikali na lugha nyingine ndio zifuate.

Akitoa maoni yake Mkurugenzi wa asasi ya Fahari ya Lugha za Afrika Juma Nyange alisema anampongeza Mbunge huyo kwani ameelezea jambo la muhimu.

“Haiwezekani sheria hizi zitungwe kwanza Kwa Kiingereza kisha ndio tuzitafsiri kwa Kiswahili. Kiswahili lazima iwe ndio lugha chanzi (source language) na lugha nyingine ndio watafsiri,” alisema Nyange.

Wanaharakati mbalimbali wa Kiswahili nao walisema lugha ya Kiswahili inao msamiati wa kutosha kutimiza lengo hilo hasa wakitolea mfano kuwa, ipo KAMUSI ya Sheria kwa Kiswahili ambayo inaweza kutoa msaada kwa kupata istalahi za kutosha za lugha ya sheria.


Author: Gadi Solomon