Mkutano wa Baraza la Mawaziri SADC kutumia Kiswahili kwa mara ya Kwanza

Peter Elias, Mwananchi
pelias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) unatarajiwa kufanyika Machi 16 na 17 hapa nchini ambapo lugha ya Kiswahili itatumika kwa mara ya kwanza kama lugha rasmi ya Sadc.

Hayo yamebainishwa Machi 2 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi wakati wa akizungumzia mkutano huo wa ngazi ya mawaziri.

Profesa Kabudi amesema mkutano huo utakaowakutanisha mawaziri wa mambo ya nje, fedha na mipango na viwanda na biashara wa Sadc, utakuwa wa mwisho kufanyika hapa nchini na mkutano ujao utafanyika Maputo, Msumbiji.

“Mkutano huu ni wa mwisho kufanyika hapa Tanzania tukiwa kama mwenyekiti wa Sadc. Mkutano ujao utafanyika Msumbiji lakini kabla ya mkutano huo, mikutano mingine ya kisekta itaendelea kufanyika hapa nchini mpaka Agosti 2020 tutakapokabidhi kijiti kwa Msumbiji,” amesema.

Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa tangu Tanzania ilipopewa uenyekiti wa Sadc, Profesa Kabudi amesema wamefanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika mikutano ya Sadc na katika mkutano huo wa Machi 16, Kiswahili kitatumika kwa mara ya kwanza.

Waziri Kabudi amesema jambo jingine walilofanikiwa ni kuondolewa kwa vikwazo kwa Zimbabwe. Amesema Serikali ya Zimbabwe inafurahishwa na hali inavyokwenda na kwamba Umoja wa Ulaya unasimakia kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

Amesema agenda ya viwanda ni jambo jingine ambalo limefanikiwa. Amesema Tanzania imekuwa nchi ya nne kuitekeleza ajenda hiyo, hivyo, imekuwa ajenda ya kudumu ya Sadc na kila nchi itakayopokea uenyekiti itakuwa na ajenda hiyo.

“Ajenda ya viwanda imekuwa ajenda ya kudumu Sadc, kinachotofautiana itakuwa ni vipaumbele tu. Sisi kipaumbele chetu ni biashara, kukuza biashara kati ya nchi na nchi. Kuna suala la ajira kupitia sekta ya viwanda na mambo mengine,” amesema Profesa Kabudi.

Kwa Ufupi
Tanzania kuongoza mkutano wa mwisho wa Baraza la Mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kuanzia Machi 16 – 17. Mkutano ujao wa Baraza hilo utafanyika Msumbiji ukifuatiwa na mkutano wa wakuu wa nchi wa Sadc utakaofanyika nchini humo, Agosti 2020.

Author: Gadi Solomon