Mwanzilishi wa Swahili Hub Profesa Ken Waribora afariki dunia

Mmoja wa waanzilishi wa Swahilihub na mtunzi mashuhuri wa vitabu, Profesa Ken Waribora amefariki dunia kutokana na ajali.

Profesa Waribora ni mmoja wa watu waliokuwa wakiisimamia na kuiendesha Swahili Hub ilipokuwa Nation Media Group (NMG) kabla ya yeye kuacha kazi na kisha baadaye Swahili Hub ilihamishiwa majukumu yake kwenye Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) nchini Tanzania.

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha mwandishi Prof Ken Walibora. Rais amemtaja kuwa mwandishi na mtangazaji shupavu ambaye kazi yake itaendelea kuvutia vizazi vijavyo.

 Waandisi, wanahabari, wapenzi na wahakiki wa Kiswahili vilevile Wakenya kwa jumla vilevile wanaendelea kumwomboleza  mwandishi  huyo tajika, mwanahabari, mtangazaji na mhakiki wa Kiswahili, Prof Ken Walibora Waliaula.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa baada ya mwili wake kupatikana katika chumba cha Maiti ya Hospitali ya Kenyatta siku kadhaa  baada ya kutoweka.

Ken alitoweka Ijumaa huku baadaye  ikibainika kwamba aliaga dunia baada ya kugongwa na basi katika Barabara ya Landhies hapa Nairobi.  Taarifa hiyo ikizua majonzi kwa wapenzi wa Kiswahili duniani.

Ofisa wa Mawasiliano katika Hospitali ya Kenyatta, Ezekiel Gikambi ni miongoni mwa waliokuwa na jukumu la kuutafuta mwili wake hadi ulipopatikana.

Ken atakumbukwa kwa mengi lakini zaidi kwa kuandika riwaya kadhaa kama Siku Njema, Kidagaa kimemwozea, damu nyeusi na kadhalika japo riwaya ya Siku Njema ndiyo iliyotambulika kwa wengi. Ken ni mwanahabari wa muda mrefu na aliyewahikuwa msomaji taarifa kabla ya kwenda Marekani kwa masomo zaidi na kurejea akiwa Profesa.

Hadi kifo chake alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Riara, Mhariri na mwandishi wa riwaya na hadithi kadhaa zinazochambuliwa hivi sasa.

Marehemu atakumbukwa kwa riwaya maarufu, Siku Njema iliyotahiniwa, Riwaya ya Kidagaa Kimemwozea na Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine vyote vilivyotahiniwa, vingine ni Nasikia Sauti ya Mama, novela ya Ndoto ya Amerika n.k. Alikuwa ameandika zaidi ya vitabu 30, makala mbalimbali vyuoni na magazetini, kuhudhuria makongamano mengi ndani na nje ya nchi.

Author: Gadi Solomon