Mzee Hega afariki dunia, kuzikwa Kibaha

Gadi Solomon, SwahiliHub

Nguli wa Kiswahili Mzee Suleiman Hega (83) amefariki dunia leo Jumatatu saa mbili asubuhi katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa familia Mohamed Hega ambaye ni mtoto wa marehemu amesema baba yao amefariki dunia kutokana na shambulio la moyo jambo ambalo awali kabla mauti hayajamfika ilimlazimu kulazwa katika chumba cha uangalizi maalumu.

Mohamed amesema msiba wa Mzee Hega upo nyumbani kwa marehemu Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam na taratibu za mazishi zinafanyika ili kwenda kupumzisha kwenye shamba lake Boko Timiza kesho saa saba mchana, Kibaha mkoani Pwani.

Mzee Hega ambaye alikuwa mwandishi nguli, pia ndiye alikuwa mwendeshaji wa kipindi cha “Ulimwengu wa Kiswahili” katika Televisheni ya Taifa (TBC1).

Aidha amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa miaka tofauti tofauti na pia alikuwa mjumbe wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) kwa vipindi mbalimbali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Ahmad Sovu amemwelezea Mzee Hega kuwa wakati wa uhai wake amekuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili

“Ama hakika sote tu waja wa Mwenyezi na kwake ndio marejeo yetu. Makiwa. Tunaomba mola wetu mtukufu ampe kauli thabiti amina,” alisema Dkt Sovu.

Mzee Hega (aliyevaa miwani) akiwa na manguli wengine wa Kiswahili enzi za uhai wake.

Naye mwanajumuiya ya Kiswahili kutoka nchini Kenya, Vikita Yusufu amewapa pole wale wote walioguswa na msiba huo.

“Kwa niaba ya Jopo la Kiswahili ninatumia fursa hii kutuma risala zetu za rambirambi kwa familia, ndugu na marafiki, BAKIZA na Wazanzibari wote kufuatia mauko ya Mzee wetu Bwana Hega. Waama, mchango wake adhimu katika Kiswahili kitasalia milele kwa wapenzi wote wa lugha hii nyerezi. Tunawaombea ili mwe na subira katika wakati huu mgumu. Mungu awape amani ya akili. Ipo siku tutamwona mzee tena,”alisema.

Author: Gadi Solomon