Namibia kuanza kufundisha Kiswahili mwakani

Kifupi: Kiswahili kitaanza kufundishwa kama somo la hityari katika shule mbalimbali za umma nchini Namibia mwakani. Hikli linakuja baada ya mipango kadhaa kufanywa na wizara ya elimu huku motisha ikiwa ni ziara iliyofanywa na Rais John Magufuli mwezi Mei mwaka jana.

WINDHOEK. Wizara ya Elimu nchini Namibia imesema kuwa itaanzisha somo la lugha ya Kiswahili katika shule zake za umma kama somo la hiyari. Hayo yalisemwa jana na Mtendaji Mkuu wa Wizara hiyo, Sanet Steenkamp akiongeza kuwa mwaka huu utatumika kufanya tathmini na kuandaa mikakati mbalimbali kwa ajili ya mpango huo.

“Wizara itatumia mwaka huu kuweka mipango katika mstari katika kuhakikisha kwamba tunaanzisha mafunzo ya lugha hii inayozungumzwa Zaidi kuliko lugha nyingine yoyote ya Afrika katika shule za Namibia.”

Gazeti la New Era la Namibia liliandika hapo jana kuwa, mwaka jana baraza la mawaziri liliiagiza Wizara ya Elimu kufungua milango yote na kuhakikisha lugha adhimu ya Kiswahili inaingizwa katika mtaala wa elimu na kuanza kufundishwa. Taarifa zinaeleza kuwa mpango wa kuanza kufundisha Kiswahili nchini humo ulichochewa zaidi na Rais wa Tanzania, John Magufuli alipofanya ziara nchini Namibia kwa kupendekeza Kiswahili kifundishwe kama somo la hiyari nchini humo.

Wakati wa ziara ya kikazi nchini Namibia mwaka jana, Rais Magufuli alipendekeza kuwa, kuanzishwa kwa ufundishaji wa Kiswahili nchini humo kutaondoa baadhi vikwazo katika biashara na kukuza uhusiano bora Zaidi baina ya nchi hizo mbili na nyinginezo.

“Kwa ujumla, suala la kuanzisha ufundishaji wa Kiswahili lilijadilia mwezi Desemba wakati wa kikao cha baraza. Tuliangalia namna ambavyo tunaweza kuanzisha somo la Kiswahili na moja ya mkakati mkuu ni kuanzisha katika shule chache kwanza ili tuone matokeo yake,” alisema Steenkamp.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa lugha yenye asili ya Afrika kutoka nje ya Namibia kufundishwa katika shule za nchi hiyo. Kimsingi, SADC imeshapitisha matumizi ya lugha ya Kiswahili mwaka jana sio tu kama lugha ya rasmi lakini pia kama lugha ya mawasiliano ndani ya Jumuiya ya SADC Nyanja za kibiashara, mazingira na nyinginezo.

Namibia inakuwa miongoni mwa nchi za kusini mwa Afrika kutangaza kufundisha Kiswahili baada ya Afrika Kusini kutangaza kufundisha Kiswahili mapema mwaka jana. Hata hivyo, Zimbabwe iliwahi kutangaza mpango huo wa kuanza kufundisha Kiswahili katika shule za nchi hiyo tangu mwaka 2016.

Kiswahili ni moja ya lugha za Kibantu yenye muundo na sifa za kiisimu zinazolandana na lugha nyingi za Kibantu zinazozungumzwa barani Afrika. Ni lugha ya kwanza kwa watu wa Pwani ya Afrika Mashariki.

Pia, Kiswahili ni lingua franka ya nchi za Maziwa Makuu na sehemu nyinginezo za Mashariki na Kusini mwa Afrika ikijumuisha Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Author: Amani Njoka