Serikali ya Canada yapitisha Siku ya Kiswahili

Gadi Solomon, Swahili Hub

Serikali ya Canada imeitambua rasmi Jumuiya ya Wazungumzaji Lugha ya Kiswahili na kutangaza Juni 22 kila mwaka itakuwa maadhimisho ya Kiswahili nchini humo.

 Akizungumza kupitia kupindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la BBC Swahili mwishoni mwa wiki iliyopita Ijumaa Juni 27, mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Waswahili nchini Canada, Amani Bagende alisema wanajumuiya hao walianza kuitangaza lugha hiyo ili iweze kufahamika jambo lililosababisha mamlaka za juu kuitambua.

Alisema kwamba waliisahjili Jumuiya hyo kwa lengo la kufanya kazi kihalali. Wanajumuiya hao walipendkeza pia kwamba wapewe siku maalumu ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili ili kuwakusanya wazungumzaji na wapenzi wa lugha ya Kiswahili.

Bagende alisema hiyo ni fursa kwa wageni na wazungumzaji wa Kiswahili kukutana na kusherehekea kwa pamoja ikiwa ni pamoja na wageni kujifunza utamaduni wa lugha ya Kiswahili.

Alisema baadhi ya mambo ambayo yatakuwa yanafanyika kwenye siku ya Kiswahili nchini humo, ni pamoja kuonyesha utamaduni wa Kiswahili na Mswahili. Pia kuchoma nyama, kupika sukuma wiki na kuonyesha ugali na burudani zingine za asili.

Lugha ya Kiswahili kwa sasa inatajwa kuwa na wazungumzaji wa asili kati ya  milioni 100-150, pia kuna watu takaribani milioni  98 wanaozungumza lugha ya Kiswahili wasio na asili ya Waswahili.

Pia, nchini Canda hadi sasa kuna  jumla ya wazungumzaji 6,000 mchanganyiko wa watu kutoka sehemu mbalimbali duniani pamoja na wenyeji.

Lugha ya Kiswahili kwa sasa ni lugha ya Taifa nchini Tanzania, Kenya, Uganda na DRC . Vilevile lugha hiyo imeingizwa kwenye mtalaa wa kufundishia katika nchi za Afrika Kusini, Rwanda na  Sudan Kusini.

Nchi zingine za Afrika ambako Kiswahili kinazungumzwa ni Malawi, Somalia, Zambia, Msumbiji, Comoro na Afrika Kusini.

Author: Gadi Solomon