Spika Ndugai: Inawezekana Bunge la Kenya kutumia Kiswahili

Gadi Solomon na Amani Njoka, Swahili Hub

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai leo Alhamisi Oktoba 31 amezindua Kanuni za Kudumu za Bunge la Kenya za lugha ya Kiswahili hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge hilo.

Tukio hilo la kihistoria lililorushwa na vituo mbalimbali vya runinga, liliambatana na wenyeviti wa kamati mbalimbali za Bunge kuwasilisha ripoti za utendaji wa kamati zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Spika Ndugai alisema Bunge la Tanzania linatumia lugha ya Kiswahili kwenye shughuli zake hivyo hata kwa Wakenya hilo linawezekana.

“Nawapongeza kwa uzinduzi huu, sasa vikao vya kamati mbalimbali vitapeperushwa mubashara,” alisema Spika Ndugai.

Bunge la Kenya limekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili miaka ya hivi karibuni lilipitisha Kiswahili kuwa lugha ya Taifa nchini humo.

Naibu Spika wa Bunge la Kenya, Moses Cheboi alisema wajumbe wa kamati mbalimbali wanapenda kutumia Kiswahili hivyo jambo hilo limewashawishi kuamua kuunda kanuni za kudumu za Bunge.

“Kutokana na wabunge wengi wanapenda kutumia Kiswahili jambo hilo limetusukuma kuunda kanuni za kudumu ambazo zitatumika kuanzia mwezi wa pili mwaka 2020,” alisema Naibu Spika Cheboi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango.

Alisema wanasiasa nchini humo wamekuwa wakifanya kampeni na kuomba kura kwa lugha ya Kiswahili. Hivyo Bunge limeona umuhimu wa kuwa na kanuni za kudumu za Kiswahili za Bunge la Kitaifa.

Author: Gadi Solomon