Tamasha la Kiswahili lafana Marekani

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Tamasha hilo lilihudhuriwa na watu mbalimbali wenye asili ya Afrika Mashariki na wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili. Mamlaka ya mji wa Prince George, Maryland ilikitunuku chama cha SSUSA kwa mchango wake kwa jamii kwa kusaidia kuwainua watu kiuchumi.

Maryland, Marekani. Hatimaye tamasha la Swahili Society Usa limekamilika juzi, Jumamosi tarehe 2/11/2019 huku likifanyika kwa mafanikio makubwa. Katika tamasha hilo masuala mbalimbali yahusuyo Kiswahili, utamaduni na hatma za Waswahili waishio Marekani.

Tamasha hilo lilihudhuriwa na Balozi Liberata Mulamula kutoka Taasisi ya Lugha za Kigeni, Chuo Kikuu cha George WashIngton aliyekuwa mgeni rasmi. Kulikuwa na matumbuizo mbalimbali, ngoma pamoja na chakula cha jioni huku mijadala kuhusu hatima yao ikiwemo kuwakwamua kiuchumi kwa kuwapa misaada mbalimbali wale wote ambao maisha yao hayana ustawi mzuri ikipamba moto.

Wasanii maarufu waliohudhuria ni; Masanja Mkandamizaji, Roma Mkatoliki na mchekeshaji, Mr Beneficial ambapo walitoa burudani ya nyimbo mbalimbali za Kiswahili na vichekesho. Masanja Mkandamizaji na Roma waliwaburudisha waliohudhuria kwa nyimbo zao kadhaa huku Mr Beneficial akitoa burudani ya aina yake. Pamoja na wasanii hao, pia zilipigwa nyimbo za wasanii kama Belle 9, Z Anti, Mez B, TID na nyinginezo za Kiswahili.

Swahili Society Usa ni taasisi iliyoanzishwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wazungumzaji na watu wote wenye asili ya Afrika Mashariki kujadili masuala mbalimbali yahusuyo utamaduni wao pamoja na masuala mengine ya kiuchumi. Kwa kutambua hilo ofisi ya mji wa Prince George imekitunuku chama hicho cheti cha kutambua mchango wake mkubwa katika kuiimarisha jamii ya Waswahili pamoja na maisha yao kiuchumi na kiutamaduni na hivyo kuimarisha maisha ya jamii yote.

Author: Gadi Solomon