Tuzo za Kiswahili Mabati-Cornell Fasihi ya Afrika kutoa mamilioni kwa washindi

Gadi Solomon

Kwa mara nyingine waandishi wa kazi za fasihi wamekaribishwa kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo ya Kiswahili ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka huu.

Lengo la tuzo hizo ni kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza Sanaa ya tafsiri kutoka lugha za Kiafrika baina la lugha za Kiafika.

Mshindi wa kwanza wa Riwaya na Ushairi kila mmoja  atajizolea zawadi ya Dola 5,000, huku mshindi wa pili wa utanzu wowote ataondoka na Dola 3,000 pia mshindi wa tatu wa utanzu wowote atajizolea Dola 2,000.

Jumla ya fedha hizoza zawadi  kwa washindi wote inafikia takribani Shilingi 34,440,000 milioni  kwa kiwango cha Dola 1= Sh2,296.

Waandaaji wa tuzo hizo wametoa mwongozo kuwa  muswada utakaoshinda, utachapishwa kwa Kiswahili na Mashirika ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota (Tanzania) na East African Educational Publishers (Kenya).

Vilevile diwani bora itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na African Poetry Book Fund.

Taarifa hiyo, inaeleza kwamba miswaada au vitabu vilivyochapishwa katika miaka miwili kabla ya tuzo inatakiwa kuwasilishwa kabla ya Agosti 5 mwaka huu.

Tuzo hiyo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 na Dk Lizzy Attre na Dk Mukoma wa Ngugi kutoka chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani.

Tuzo hizo kwa mwaka 2018, zilizotolewa Februari mwaka huu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alimkabidhi cheti cha ushindi wa tuzo ya Fasihi, Jacob  Julius sherehe zilizofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Pia sherehe hizo za utoaji tuzo zilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Author: Gadi Solomon