Ufaulu Kiswahili wapanda Kenya

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Matokeo ya mitihani kwa somo la Kiswahili yamekuwa si mazuri kwa kipindi cha hivi karibuni. Hata hivi katika matokeo ya mwaka huu wanafunzi wameonekana kufanya vizuri zaidi kulinganisha na matokeo yaliyopita.

Nairobi. Wiki iliyopita Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) lilitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya sekondari (Kidato cha nne). Akizutangaza matokeo hayo, Katibu wa Baraza la Elimu Profesa George Magoha alisema kwamba, matokeo ya mwaka huu yamekuwa mazuri kulinganisha na yaliyopita.

“Matokeo ya mwaka 2019 yanaonekana kupanda katika ufaulu wake hasa kwa masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Fizikia, Kemia, Biolojia na kwamba ndio masomo ambayo ufaulu wake umepanda zaidi mwaka huu.”

Hii ni habari ya njema kwa wadau na wapenzi wa Kiswahili kuwa somo la Kiswahili ni miongoni mwa masomo ambayo yamefanya vizuri zaidi na ni dalili kuwa Kiswahili kitaanza kuwavutia wanafunzi wengi na hatimaye wataalam kuongezeka zaidi katika siku za usoni.

Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo alisema, ufaulu wa wasichana katika masomo ya Sanaa kama Kiswahili, English, Sanaa, Kijerumani kulinganisha na wavulana. Matokeo hayo yanaonesha kuwa nafasi ya wanafunzi kufaulu kuendelea na masomo ya elimu ya juu imepanda kutoka watahiniwa 90,377 mwaka uliopita na kufikia 125,746 mwaka huu.

Sambamba na hilo, Katibu huyo alitoa pole kwa wanafunzi wote waliojiua mara baada ya matokeo ya elimu ya msingi kutangazwa kwa kuona kuwa ufaulu wao haukuwa mzuri kulingana na matarajio yao.

“Inasikitisha kuona mmoja wa wanafunzi waliojiua alipata 195 na kusema kwamba wapo wanafunzi wengi waliopata chini ya alama 200 na wamepata shule. Kama motto kama huyu emepata alama hizi na anajiua, ni alama zipi ambazo alitaka?”

Hata hivyo aliwalaumu wazazi kwa kutokuwa kuwa makini na kueleza kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwakemea watoto wao na kuwalazimisha kurudia shule au mitihani watoto wao pale wanapopata alama chini ya kiwango na kusababisha kujiua. Aliwaomba wazazi kuwatia moyo watoto kwani hakuna linaloshindikana badala ya kuwalaumu.

Pia ameomba wazazi kuwa na usimamizi wa karibu zaidi kwa watoto hasa wasichana ili wawasaidie kuepuka mimba za utotoni ambazo zimechangia kutokumaliza shule kwa kiasi kikubwa.

Author: Amani Njoka