Wanataaluma wa Kiswahili wamwandikia kitabu Profesa Madumula

Amani Njoka na Gadi Solomon, Swahili Hub

Kwa ufupi: Makala mbalimbali zinazohusu lugha na fasihi ya Kiswahili zinapatikana ndani ya kitabu hicho kiitwacho ‘Koja la Taaluma za Insia’. Zimeandikwa na wanazuoni kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Dar es Salaam. Wataalamu mbalimbali wa Kiswahili kutoka ndani nan je ya Tanzania wameandika makala za kitabu cha heshima kinachoitwa Koja la Taaluma za Insia kwa ajili ya kumtunuku Profesa Joshua Madumula.

Koja la Taaluma za Insia kimeandikwa kwa heshima ya Profesa Madumula. Kitabu hicho chenye mkusanyiko wa makala mbalimbali za Kiswahili na Fasihi ya Kiswahili kimechapishwa kwa ajili ya kusomwa na marejeleo. Pia zipo makala zinazohusu lugha (isimu) na fasihi ya Kiswahili kutoka Tanzania na sehemu nyingine ulimwenguni.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Athumani Ponera amesema kitabu hicho ni kwa ajili ya kutambua na kuuenzi mchango wa Profesa Madumula katika taaluma katika sehemu mbalimbali.

“Tuliona ni vyema tukafanya jambo ambalo litakuwa kumbukumbu nzuri kwa Profesa Madumula kwani mchango wake katika uga wa kitaaluma ndani na nje ya nchi ni wa kutukuka. Tumekuwa nyuma kwa kiasi fulani kwani tayari wenzetu Wakenya wamekuwa wakifanya hivyo, ni jambo jema., alisema Dk Ponera.

Akizungumzia kuhusu kitabu hicho, Profesa Madumula amesema ingawa hajakiona kitabu lakini nimezipata tu taarifa hizo na amefurahia.

“Ni jambo jema na nimelipokea kwa furaha, nimefurahishwa na hatua ya waandishi hao kutoa kitabu cha heshima kwa ajili yangu, ni kitu cha kufurahisha ikiwa watu wanakuzungumzia kwa uzuri,” alisema Profesa Madumula

Kitabu hicho kitakuwa ni miongoni mwa machapisho ya hivi karibuni ambayo yamesheheni makala kuhusu lugha adhimu ya Kiswahili. Pia ni mahususi kwa kada zote za kitaaluma, kuanzia ngazi za kati mpaka vyuo vikuu na kwamba wadau, wakufunzi na walimu wanaweza kukisoma kwa kuongeza maarifa.

Uzinduzi wa kitabu hicho chenye mkusanyiko wa makala takribani 32 utafanyika Desemba Mosi katika Chuo Kikuu cha Dodoma, na Profesa Madumula anatarajiwa kuwa miongoni mwa wageni wa heshima katika hafla hiyo.

Author: Gadi Solomon