Wadau Kenya waomba serikali itilie mkazo matumizi ya Kiswahili

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Nchi zilizoendelea na kukua kiuchumi kama Japan, China na Uingereza zinazitumia lugha zao za taifa. Viongozi wa kiserikali wametakiwa kutumia Kiswahili wanapokwenda kwenye mikutano ya kimataifa.

Nairobi. Wasomi, wadau, wahadhiri na waalimu wa Kiswahili nchini Kenya wameiomba serikali kuipa nguvu lugha ya Kiswahili iwe lugha pekee ya mawasiliano na shughuli mbalimbali katika sera zake ili kurahisisha mawasiliano na kuongeza kasi ya maendeleo nchini humo.

Haya yanakuja muda mfupi kufuatia maoni mengi ya wadau yaliyokusanywa na Baraza la Kiswahili la Kenya mwaka 2019 ambayo yanaeleza kuwa, mataifa mengi ambayo yanategemea lugha za kigeni kama lugha rasmi zipo nyuma kimaendeleo. Walitoa mfano wa mataifa yaliyoendelea kama vile Japan, China na Uingereza kama miongoni mwa mataifa yanayotumia lugha zao.

Waliongeza kuwa, ukuaji wa kiuchumi, kijamii na kisiasa umekuwa na kasi ndogo nchini humo kwa sababu taifa limeshindwa kuitumia vyema lugha ya Kiswahili ambayo inatambulika kikatiba kama lugha ya taifa.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Dk Jesse Muriithi alisema kasi ya ukuaji wa maendeleo ya Kenya itaonekana ikiwa tu Kiswahili kitapewa nguvu ya kutumika kikamilifu kama lugha ya mawasiliano katika shughuli zote za kitaifa, kazi mbalimbali na hata katika ufundishaji shuleni na vyuoni.

“Mambo mengi yanahitaji kufanyika kuhakikisha kuwa lugha hii inachukua nafasi inayostahili. Ninapendekeza serikali iunde utaratibu kwamba kabla mtu yeyote hajaajiriwa kuwa mfanyakazi wa umma, ni lazima afaulu mtihani wa kupimwa Kiswahili.” alisema.

Muriithi alisema kuanzishwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya kuende sambamba na kutengewa bajeti kama ilivyo kwa taasisi zingine ili liwe na uwezo wa kutosha wa kusimamia ukuaji wa lugha hiyo kwa manufaa ya mustakabali wa Wakenya wote.

Vilevile wasomi hao wa Kiswahili waliibua hoja ya Kiswahili kutokutambuliwa katika mtalaa mpya wa elimu.

Mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Mukangu, Lincorn Murithi alisema Kiswahili kimekuwa kikipewa nafasi ndogo sana katika mtalaa wa elimu ukilinganisha na Kiingereza na masomo mengine licha kuwa ndiyo lugha ambayo kila mtu anaielewa kirahisi. Aliongeza kuwa, lugha hii inapaswa ipewe kipaumbele kwani inatambulika kikatiba kama lugha rasmi.

“Inasikitisha kwamba idadi ya masomo yanayotolewa kwa Kiswahili katika mtalaa wa elimu ngazi ya msingi ni ndogo na inaendelea hivyo mpaka katika ngazi ya sekondari ambako inafanywa kama hiyari badala ya lazima kama ilivyo kwa Kiingereza ambayo ni lugha ya kigeni.”

Pia mbunge wa Manyatta, John Muchiri alitaka kuwe na msisitizo mkubwa wa matumizi ya Kiswahili katika shughuli za kiserikali. Alisema viongozi wa Kenya wanapaswa kukitumia Kiswahili hata kila wanapohudhuria mikutano ya Kimataifa kisha kitafsiriwe kwenda katika lugha nyingine kama inavyofanyika kwa viongozi wengine wa nchi kama Japan na Ujerumani.

Hivi sasa nchini Kenya kumekuwa na mwamko mkubwa kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili na kumepokelewa kwa hamasa kubwa. Mjadala huu umeibuka mwezi moja pekee baada ya Bunge la Kenya kuidhinisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli zake zote.

Author: Amani Njoka