Waserbia wapigana msasa wa Kiswahili kwao

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi: Taasisi hiyo imesema warsha hiyo ni maalum kwa ajili ya raia w3a Serbia pekee wanaojifunza lugha ya Kiswahili na warsha hiyo itahusu vipengele vyote vya lugha ambavyo ni kuongea, kusikiliza, kuandika na kusoma.

Belgrade. Makumbusho ya Sanaa za Afrika ya mjini Belgrade nchini Serbia imeandaa warsha maalum kwa ajili ya raia wake wanaojifunza kuzungumza na wanaozungumza Kiswahili kwa kiwango cha awali ili kuwapiga msasa. Warsha hiyo itawahusisha watu wenye umri wa miaka 16 na kuendelea. Warsha hiyo itaongozwa na Dk Marija Panic na Benjamin Towett Chemarum.

Mtandao wa makumbusho hayo unaeleza kuwa warsha hiyo ilianza tarehe 3 Novemba na itaendelea mpaka tarehe 29 Desemba. Warsha hiyo itawahusisha wale wote wanaojifunza Kiswahili katika ngazi ya awali na baada ya warsha hiyo watamudu kuwasiliana kwa lugha ya Kiswahili kwa kiwango cha kawaida.

Akizungumzia warsha hiyo, Dk Panic (Phd) ambaye amekuwa akifundisha Kiswahili katika makumbusho hayo tangu 2018 amesema kuwa warsha hiyo ni kwa ajili ya Waserbia pekee na kwa ajili ya kuwaimarisha hasa wale wa ngazi ya awali na kwamba usajili ulishafungwa tangu mwezi Oktoba na sasa warsha inaendelea.

Kiswahili kimekuwa rahisi kujifunza kwa Waserbia kwa kuwa mfumo wa sauti na irabu wa Kiswahili unakaribiana kwa kiwango kikubwa. Pia mtandao wa makumbusho hayo ulieleza kuwa Kiserbia kinakaribiana na Kiswahili kwa husomwa kama inavyoandikwa.

Kwa kaasi kikubwa raia wa Serbia hujifunza Kiswahili kwa ajili ya shughuli za kibiashara, safari za kawaida wanapotembelea Afrika kwa ajili ya utalii na mazungumzo pindi wanapotangamana na wazungumzaji wa lugha hii.

Author: Gadi Solomon