Maktaba ya Kiswahili kuanzishwa Zanzibar

Gadi Solomon na Amani Njoka, Swahili Hub

Zanzibar. Serikali ya Zanzibar imekiagiza Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) kuanzisha skuli ya utafiti na ukalimani ili kuweza kukidhi mahitaji ya wataalamu wa tafsiri na ukalimani kwenye mikutano ya kimataifa na kutoa wito kwa wataalamu kuanza kupelekea tasnifu zao kwa ajili ya makataba ya Kiswahili inayotarajiwa kujengwa Zanzibar.

Akizungumzungumza kwenye Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili, Mgeni rasmi, Balozi Seif Ali Idd kwa niamba ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema kutokana na Suza kuwa kitovu cha kufundisha Kiswahili kwa wageni na sasa kituo hicho kimekuwa Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni.

Alisema jambo hilo linahitaji mkakati na matumaini yake litafanikiwa kwa sababu Serikali tayari inayo wataalamu na dhamira. Pia kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuongeza wataalamu wa Kiswahili ikiwemo SUZA kuanzisha kozi ya uzamivu na tayari wamehitimu 12 mpaka sasa.

Aidha Balozi Iddi alisema, Serikali imeanza kuipitia kamusi yake ya Kiswahili ya 2010 ili kuiimarisha zaidi. Kamusi hiyo itapitiwa na kutaangalia namna ya kuboresha ili iwe bora zaidi.

Sambamba na hilo, kitabu kipya cha mashairi ya Kiswahili cha Shwari Mtunzi, kilichotungwa na mshairi mbobezi, Haji Gora Haji kimezinduliwa na Dk Shein.

Katika Kongamano hilo la tatu la Kiswahili la Kimataifa kuliwasilishwa tasnifu zaidi ya 60 ambazo zinaweza kutumika kama marejeleo ya masomo na tafiti mbalimbali za Kiswahili. Tasnifu hizo zilitoka kwa wahitimu zaidi wa 150 kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambao walihudhuria na kuwasilisha mada katika Kongamano hilo.

Upatikanaji wa makala, tasnifu, majarida na vitabu vya Kiswahili utawezesha kupatikana kwa vitendea kazi baada ya kuanzishwa na kuimarika kwa maktaba ya Kiswahili ambayo itakuwa msaada mkubwa katika tafiti mbalimbali kuhusu maendeleo ya Kiswahili.  

Author: Amani Njoka