World Academy waja na kongamano lingine la Kiswahili na Utamaduni Dubai

Amani Njoka, Swahili Hub

Kifupi:Ni kongamano ambalo wasomi na watafiti watawasilisha mada, midahalo, tafiti na matokeo ya tafiti zao kwa mapana na marefu kuhusu lugha ya Kiswahili, utamaduni wake na uhusiano wake na lugha nyingine.

Paris. Taasisi inayojihusisha na uchapishaji na uendeshaji wa makongamano mbalimbali ulimwenguni kuhusu siasa, uchumi, sayansi na teknolojia, utamaduni na masuala mengine iitwayo World Academy imeandaa kongamano kuhusu Kiswahili na Utamaduni wake.

Tovuti ya Taasisi hiyo yenye makao makuu yake mjini Paris, Ufaransa  inaeleza kuwa kongamano hilo litafanyika tarehe 17-18 Desemba, 2020 mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu. Kongamano hilo litakuwa na mada mbalimbali ambazo watafiti na wasomi wataziwasilisha. Baada ya kuwasilisha mada utafanyika mdahalo kuhusu lugha hiyo, mchango wake katika maendeleo na maisha ya kila siku kwa ujumla.

Pamoja na hayo, jarida maalum lenye mada mbalimbali za Kiswahili pamoja na fasihi litachapishwa baada ya kufanyika mchakato wa kuchuja makala au mada zilizofanya vizuri mada zilizowasilishwa ili zichapishwe ndani ya jarida hilo ambalo litaitwa Swahili Language and Culture (Lugha ya Kiswahili na Utamaduni). Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa ni pamoja na uhusiano wa Kiswahili na Kiingereza, Matumizi yake, Semantiki ya Kiswahili, Mbinu za Ufundishaji wa Kiswahili, Kiswahili mitandaoni na nyinginezo.

Hili litakuwa kongamano la pili kuhusu Kiswahili kuandaliwa na Taasisi hii kwa mwaka 2020 kwani tayari imeandaa kongamano lingine kubwa kuhusu ambalo litafanyika Roma, Italia tarehe 12-13 Desemba 2019. Katika kongamano la Desemba mwaka 2019, mada nyingi pia zitawasilishwa.

Kumeshuhudiwa makongamano mengi ya ndani na nje ya nchi za Afrika Mashariki baada ya kuona kuna haja ya kukitumia Kiswahili katika maeneo mbalimbali ya maisha ya binadamu. Hivi sasa Kiswahili kina istilahi za kutosha katika biashara, elimu, sayansi na teknolojia na kinazungumzwa na watu wengi na hivyo kuzidi kuwashughulisha wataalam wa lugha na wasomi ili kuona kama kinaweza kutumika zaidi katika jamii nyinginezo.

Kwa habari zaidi tembelea>>> https://waset.org/swahili-language-and-culture-conference-in-december-2020-in-dubai

Author: Gadi Solomon