Mawimbi

Patrick J. Massawe

Utangulizi.

Fred Samson kijana mtanashati anakutana ndani ya basi la daladala na mwanadada mrembo, Mariana, wakati huo mvua kubwa inayesha upande wa nje. Lakini wanapofika mwisho wa safari yao, Mariana anamsitiri kumfunika kwa mwavuli wake ili asilowane.

Hatimaye wanaongozana wote huku wakitambulishana, na safari yao inaishia kujenga uhusiano mzito wa kimapenzi ambao baadaye unaleta misukosuko mingi na karaha na kuhatarisha penzi lao! Endelea na hadithi hii ya kusisimua mpaka mwisho wake….

MVUA za masika zilikuwa zinaendelea kunyesha mfululizo ndani ya jiji la Dar es Salaam, na kulifanya liwe katika utulivu wa hali ya juu.  Ni mvua ambazo pia zilibadilisha hali ya hewa yenye joto jingi na kuwa ya ubaridi, iliyowafanya watu wengi waliokuwa wameyachimbia makoti yao masandukuni, wayatoe na kuyavaa.

Mvua hiyo kubwa ikiendelea kunyesha upande wa nje, ndani ya basi la daladala linalofanya safari zake kati ya Tegeta, Mwenge, na Posta, kijana mtanashati, Fred Samson, alikuwa ni mmoja wa abiria waliokuwa wanaelekea katikati ya jiji katika mihangaiko asubuhi hiyo ya aina yake.

Hakika hali hiyo iliyoko huko nje, ilikuwa ilimfanya Fred ajifikirie hatima yake, yaani baada ya kufika mwisho wa safari yake, eneo la Posta Mpya, mtaa wa Azikiwe, atashukaje? Maana ni lazima atalowana kwa vile hakuwa na mwavuli wa kujisetiri na mvua hiyo iliyokuwa inaendelea kunyesha kwa kasi.

Kwanza kabisa Fred alijiangalia. Alikuwa amevalia nguo nadhifu, shati lake jeupe la mikono mirefu lililosindikizwa na tai yenye rangi ya mchanganyiko. Chini alivalia suruali nyeusi iliyonyooshwa vizuri kwa pasi, na miguuni alivalia viatu vyeusi vya ngozi vilivyong’arishwa kwa rangi ya viatu.

Sasa vyote aliona ni kazi bure kwa sababu atalowana na kuchafuka kutokana na maji ambayo yatakuwa yametuama barabarani kwa vile miundo mbinu ilikuwa mibovu. Asubuhi hiyo Fred alipotoka nyumbani kwake, eneo la Mwenge, mvua ilikuwa haijaanza kunyesha ingawa wingu zito lilikuwa limetanda angani na kutishia hali ya hewa.

Lakini alijua kuwa angeweza kuiwahi na kufika mjini bila mvua hiyo kunyesha, lakini kinyume chake ndicho hicho kinachoendelea. Sasa hicho ndicho alichokuwa anawazia Fred, ukizingatia alikuwa anakwenda ofisini asubuhi hiyo.

Je, akilowana ataweza kuhimili kushinda na nguo zake zilizolowa maji kutwa nzima, huku akipishana na wafanyakazi wenzake watakaokuwa wanamshangaa? Hakika asingeweza!

Daladala liliendelea kuchapa mwendo kuifuata Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, huku likipita katika vituo kadhaa, ambapo hakuna hata abiria aliyepanda, kutokana na wengi kujificha ili kujisetiri wasilowane na mvua. Abiria waliokuwa ndani ya daladala hilo, wote walikuwa wamenyamaza kimya, bila shaka nao walikuwa wakiwaza kama alivyokuwa anawaza yeye!

Upande wake wa kushoto dirishani,  alikuwa amekaa mwanadada mmoja, mrembo wa haja, ambaye naye alikuwa amenyamaza kimya. Alikuwa akiangalia nje jinsi mvua hiyo ilivyokuwa inaendelea kunyesha kwa kasi ya ajabu.

Ni mwanadada aliyekuwa amevalia nadhifu, nguo yake aina ya suti ya kike ya rangi ya pinki, iliyomkaa vyema, na kichwani alikuwa amezisuka nywele zake mtindo wa rasta za kimasai, zilizoendana na sura yake jamali.

Fred alikuwa akisikilizia harufu nzuri ya manukato ya bei mbaya, aliyokuwa amejipulizia, ambayo haikukera katika tundu zake za pua. Alikumbuka kuwa mwanadada huyo alikuwa amepandia mwanzo kabisa, kwenye kituo cha daladala cha Bamaga, ambapo waliongozana wote kupanda, na hatimaye wakajikuta wamekaa kwenye kiti kimoja, yeye akiwa upande wa dirishani.

Fred aliendelea kumwangalia mwanadada huyo, na kumwona alikuwa amejiandaa vya kutosha. Mkononi alikuwa ameshika mwavuli mmoja mkubwa, ambao kwa muda ule ulikuwa umefungwa na hakuwa na wasiwasi wowote. Bila shaka naye alikuwa anamsikitikia kwa kutokuwa na mwavuli wa kujisetiri na jinsi alivyoonekana ni kijana mtanashati. Akiwa ni mtu mcheshi na anayependa kuongea na watu, alimwangalia mwanadada huyo na kumwambia:

“Aisee, mvua kubwa inanyesha?”

“Ni kweli. Mvua ni kubwa, huu ndiyo msimu wake…” mwanadada huyo alimjibu Fred huku akiendelea kuangalia mbele.

“Hii ni balaa sasa!” Fred akamwambia huyo, halafu akamwambia kwa sauti ndogo,

“Aisee, mvua inanyesha  kweli huko nje…”

huku akifyonza.

“Balaa gani tena? Hii ni Baraka kaka…” mwanadada huyo akamwambia huku akitabasamu.

“Ninasema hivyo kwa sababu, sijui itakuwaje nitakapofika mwisho wa safari yangu,  Posta Mpya. Ni lazima nitalowana tu…” Fred aliendelea kumwambia, akionyesha kama kujutia kwa kutokuwa na mwavuli.

“Ni kweli, lazima ulowane, maana hii mvua siyo ya kukatika muda huu…” mwanadada huyo akamwambia na kuendelea. “Lakini usijali sana, nitakusaidia kaka’ngu. Hapa nilipo nina mwavuli mkubwa.”

“Oh, ninashukuru sana, hakika nina bahati ya mtende kukaa na wewe…” Fred alimwambia huku akitabasamu. Alikuwa na matumaini ya kunusurika kulowana na mvua hiyo.

“Ndiyo hivyo kaka’ngu,” mwanadada akamwambia na kuongeza. “Kwa leo una bahati kwelikweli…”

“Kweli nina bahati ya pekee,” Fred akamalizia kusema huku akijichekesha.

Mwanadada huyo naye akabaki akitabasamu!

Safari ikaendelea kwa mwendo wa kinyonga huku daladala hilo alilopanda likipambana na foleni kubwa na ya kukera kutokana na mvua hiyo iliyokuwa inanyesha, kwani hata wale Askari wa Usalama Barabarani, nao walikuwa wamejibanza sehemu zenye vivuli, kwa kuhofia kulowana. Nidhamu ya madereva nayo ilishuka na kujikuta wakishindwa kuzingatia sheria.

      ********

Hatimaye walipofika kwenye Kituo cha Daladala cha Posta Mpya, Barabara ya Azikiwe, katikati ya jiji la Dar es Salaam. Baada ya daladala kusimama kituoni, kila mtu alibaki amekaa kwenye kiti chake, bila kushuka kwa wale ambao hawakuwa na miavuli.

Fred naye akawa ni mmoja wao, akabaki akimwangalia mwanadada yule, ambaye kabla ya kushuka, aliufungua mwavuli wake!

“Twen’zetu kaka…” mwanadada huyo akamwambia.

“Sawa, dada’ngu…” Fred  akasema huku akinyanyuka kutoka kitini kumfuata mrembo huyo wa nguvu.

Wote wawili walishuka chini huku wamejifunika ule mwavuli mkubwa, na kuepuka kulowana na mvua hiyo iliyokuwa bado inaendelea kunyesha. Baada ya kufika chini, walienda kubanisha katika baraza ya Jengo la Shirika la Posta, lililoko jirani na kituo kile cha daladala. Hapo palikuwa na watu wengi waliojibanza kujisetiri.

“Oh, nashukuru sana…” Fred akamwambia mwanadada huyo huku wakiwa wamesimama katika baraza ya Benki ya Posta.

“Unashukuru kabla hujafika unapokwenda? Si unaona mvua bado inaendelea kunyesha?” Mwanadada huyo alimwambia huku akitabasamu.

“Hakuna jinsi, nitafanyeje?” Fred akamwambia kana kwamba alikuwa anahitaji msaada mwingine kutoka kwake.

Na ndivyo ilivyokuwa!

“Kwani unaelekea wapi?” Fred akamuuliza.

“Mimi naelekea kazini, “ mwanadada huyo akamwambia na kuendelea. “Ofisi ninayofanyia kazi iko katika mtaa wa Mirambo…”

“Oh, vizuri sana. Hata mimi naelekea mtaa wa Sokoine Drive, sehemu ambayo ninafanyia kazi. Usijali, nitakupa lifti…”

“Ubarikiwe dada’ngu…” Fred akamwambia.

“Usijali, binadamu lazima wasaidiane…”

Baada ya kusimama katika eneo lile kwa muda, mvua ilipungua kiasi cha kuwapa fursa watu waweze kuondoka katika vibaraza vya majumba. Pia, Fred na mwanadada huyo waliondoka huku wamejifunika ule mwavuli mkubwa.

Wakaufuata mtaa wa Garden huku wakipigana vikumbo na wapiti njia ambao nao walikuwa wakiikimbia ile mvua hadi walipofika usawa wa Imalaseko Supermarket, ambapo walipinda kulia, na kuufuata mtaa wa Pamba moja kwa moja hadi walipoukuta mtaa wa Sokoine Drive.

“Mimi nimefika kaka’ngu…” mwanadada akamwambia Fred kwa sauti ya kinanda huku akimrembulia macho yake mazuri.

“Umeshafika siyo?” Fred akamuuliza huku akionyesha shukrani ya kusaidiwa, na pia akiushangaa ule uzuri wake!

“Ndiyo, nafanyia kazi kwenye Jengo la Sukari House, ghorofa ya tatu…” mwanadada akamwambia.

“Basi, nashukuru sana,” Fred akamwambia na kuendelea. “Lakini kutokana na wema wako. Naomba tufahamiane angalau, kwani ni watu wachache sana, hususana wanawake wenye huruma kama wewe…”

“Ni kweli, kufahamiana ni vizuri. Mimi kwa jina naitwa Mariana Mkonyi, nafanya kazi kwenye Kampuni ya Wakala wa Usafiri wa Ndege…”

“Nashukru sana, na mimi naitwa Fred Samson, ni Mwandishi wa Habari. Ninaafanya kazi katika gazeti la kiswahili, la ‘Mbantu,’ na ofisi yetu iko katika mtaa wa Mirambo…”

“Nami nashukuru kukufahamu.”

“Ahsante sana. Lakini ni vizuri pia, tukipeana namba za simu.”

“Ni jambo la maana.”

Wakiwa bado wamesimama pale barazani, walipeana namba za simu za mkononi, wakitegemea kuwasiliana tena kwa kufahamiana zaidi. Baada ya kumaliza kupeana namba, wakaachana, ambapo Mariana alielekea katika Jengo la Sukari House, na Fred akaufuata mtaa wa Sokoine kuelekea ofisi kwake.

Wakati huo mvua ilikuwa imeshakatika kabisa na hali kuwa shwari. Watu wakaanza kuelekea katika shughuli zao makundi kwa makundi.

      ********

Fred  alifika katika ofisi ya gazeti la Mbantu, iliyokuwa katika jengo moja la ghorofa saba, lililoko katika mtaa wa Mirambo, ambapo ofisi yao ilikuwa katika ghorofa ya tatu. Ni jengo ambalo lilijulikana kwa jina la Kipepeo Tower, ambapo kulikuwa na ofisi za taasisi na makampuni mbalimbali yaliyokuwa yemepanga mle.

Fred hakupenda kutumia lifti, isipokuwa alipanda kwa kutumia miguu ambao ni utaratibu aliokuwa ameuzoea siku zote, kwa kile alichokita ni moja ya kufanya mazoezi. Baada ya kuingia ofisini,  alisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wenzake aliowakuta wameshafika.

Waliongea mawili matatu huku wakiizungumzia ile mvua iliyoanza kunyesha kuanza alfajiri ya siku hiyo. Kwa kawaida mvua inaponyesha ndani ya jiji la Dar es Salaam, wafanyakazi wengi, ambao wanakaa maeneo ya mbali nje ya jiji, huwa wanachelewa kazini hasa ukizingatia foleni ya magari inasumbua sana mabarabarani.

Ndiyo maana siku hiyo walikuwa wamefika wachache tu, akiwemo yeye Fred. Alipomaliza kuongea na wafanyakazi wenzake, Fred alielekea katika meza yake na kujiandaa kuanza kazi ya siku ile. Alichapa kazi kama ratiba yake ilivyokuwa imepangwa, na kumalizia baadhi ya viporo vilivyokuwa vimebaki jana yake.

Yeye alikuwa ni mhariri wa makala katika gazeti lile la Mbantu, ambalo ni moja ya magazeti mengi yaliyochipukia hapa nchini, likiwa katika orodha ya magazeti yanayoandika hyabari mchanganyiko, za kisiasa, kiuchumi, kijamii na burudani .

Hata hivyo pamoja na Fred kuendelea na kazi, kuna kitu kimoja kilichokuwa kinamsumbua sana katika mawazo yake. Ilikuwa ni juu ya kimwana yule waliyekutana naye ndani ya basi la daladala, ambaye alimfahamisha kwa jina la Mariana Mkonyi.

Ingawa alimwona kwa muda mchache tu, moyo wake ulitokea kumpenda, kutokana na ile hali ya ucheshi, uungwana, na huruma aliyokuwa amemwonyesha siku ile.

Ukweli ni kwamba tokea Fred awe mtu mzima, abalehe na kuelewa kuhusu wanawake, hakuwahi kukutana na mwanamke mwenye huruma kama yule aliyekutana naye muda ule.

Baadhi ya wanawake wengine huwa hawana huruma ingawa ni mama zetu waliotuzaa, hujiona kama wao ni wanyonge na wanaopaswa kusaidiwa tu, na si vinginevyo. Wengine wanataka kujilinganisha na wanaume kwa kutaka usawa, hamsini kwa hamsini, ni kitu ambacho kwa nadharia inawezekana, lakini si kwa vitendo!

*******

Kivuli cha mwanadada mrembo, Mariana, kiliendelea kumsumbua Fred  kichwani mwake, ingawa mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana kwa simu. Katika mawasiliano yao, ndipo walipopanga siku moja kukutana katika mazungumzo ya faragha katika kufahamiana zaidi.

Walipanga kukutana siku ya Jumapili moja, katika Hoteli ya Amazon, iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam. Hii ni hoteli nadhifu iliyoko katika mtaa wa Jamhuri, ambayo hutembelewa na watu wa aina mbalimbali, wakiwemo hata wa mataifa ya nje, kutokana na huduma zake nzuri.

Ahadi ile ilitimizwa kwa wote kufika katika eneo husika kama walivyopanga. Mtu wa kwanza kufika pale hotelini alikuwa ni Fred ambaye alifika kunako majira ya saa kumi za jioni, kwa usafiri wa teksi.

Mara baada ya kufika, aliingia ndani ya hoteli hiyo na kwenda kukaa sehemu yenye utulivu wa hali ya juu iliyokuwa upande wa nyuma wa hoteli hiyo.

Ni sehemu iliyokuwa wazi ambapo unaweza kuiona anga, na pia palikuwa na viti vilivyokuwa vimepangwa katikati ya bustani iliyokuwa na miti pamoja na maua ayaliyozunguka eneo lote.

Fred aliagiza kinywaji alichokuwa anapendelea kwa muda ule, ambpo aliagiza mvinyo mweupe aina ya Penasol, pamoja na korosho mbichi. Akaendelea kunywa taratibu huku akitafuna korosho.

Muda siyo mrefu, Mariana naye aliingia ndani ya hoteli hiyo na kumfuata Fred pale alipokaa baada ya kumjulisha kwa simu. Alipokaa tu, naye Mariana alihudumiwa kinywaji, mvinyo mwekundu aina Dompo, ambao alikuwa anapendelea kunywa.

Wakaendelea kunywa huku kila mmoja akiwa na mawazo yake kichwani. Tuseme kila mmoja alipanga jinsi ya kuanza yale mazungumzo yao yaliyowakutanisha pale, jioni ile.

Pale walipokuwa wamekaa, Fred na Mariana walionekana kama wapenzi wawili, ambapo waliongea mengi sana yanayohusu maisha kwa ujumla, huku wakiendelea kujipatia vinywaji vya kusuuza makoo yao, na baadaye waliagiza chakula, chipsi kwa nyama ya kuku wa kuchoma, wakaendelea kula.

Baada ya kuongea mengi, kimya kifupi kilitawala kwa muda huku wakimalizia chakula chao. Fred aliyekuwa na hamu kubwa ya kuyaanzisha mazungumzo, alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, kisha akaanza kujitambulisha kwa Mariana, ambapo alimwita kwa sauti ndogo ambayo iliweza kusikika vizuri masikioni mwa Mariana:

“Mariana…”

“Bee…” Mariana aliitikia kwa sauti ndogo.

“Unajua sasa yapata mwezi mmoja tangu tufahamiane, sivyo?”

“Ni kweli kabisa, ni mwezi sasa…” Mariana alimjibu.

“Lakini ni vizuri tukafahamiana zaidi kiundani…” Fred alimwambia huku akimwangalia.

“Tufahamiane kiundani?” Mariana akamuuliza huku akimwangalia.

“Ndiyo. Kufahamiana zaidi,  kihistoria pia, umezaliwa wapi, kabila gani, umesomea wapi na kadhalika…natumaini umenipata,” Fred akamwambia kwa kumfafanulia zaidi.

“Basi, hakuna shaka…nimekuelewa…” Mariana akasema huku akiunda tabasamu pevu kiasi cha kufanya meno yake yenye mwanya yaonekane, na pia matundu mawili yaonekane katika pande zote za mashavu yake.

“Vizuri, mimi naitwa Fred Samson Makweba, nina umri wa miaka 35, nimesoma mpaka kidato cha sita, nina Shahada ya Kwanza ya Taaluma ya Uandishi wa Habari, niliyosomea katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Mtakatifu Agostino, jijini Mwanza.

Ninafanya kazi kwenye gazeti la ‘Mbantu,’ kama mwandishi wa habari, bado sijaoa, na sina mchumba…” Fred akamwambia Mariana huku akimwangalia kwa makini, lakini Mariana aliyakwepesha macho yake na kuangalia kando.

“Nashukuru sana kwa utambulisho wako,” Mariana alisema na kuendelea. “Mimi naitwa Mariana John Kwayu, nina umri wa miaka 27, nimezaliwa hapa hapa jijini Dar es Salaam, kabila langu ni Mchagga. Nimesoma mpaka kidato cha sita, na baada ya kumaliza, nikaajiriwa kwenye Kampuni ya Wakala wa Usafiri wa Ndege, sijaolewa na wala sina mchumba.

Lakini kuna jamaa mmoja ambaye ananifuatilia sana na kuomba uchumba na mimi, hata hivyo siyo chaguo langu, na wala sijampenda…” Mariana akamaliza kusema.

“Nashukuru sana kwa kunifahamisha hayo yote. Lakini pamoja na kunitambulisha, na mimi napenda kukujulisha juu ya huu wito wangu wa kuja kukutana hapa,” Fred alimwambia.

“Unataka kunieleza nini?” Mariana akamuuliza.

“Bila kuficha, tokea siku ile tulipokutana ndani ya daladala halafu ukanisaidia kunikinga na mvua, basi mpaka leo, umekaa ndani ya moyo wangu.

Tambua mimi ni mwanaume, nielewe, nimevumilia lakini nimeshindwa!” Fred alimwambia Mariana kwa sauti ya upole iliyoonyesha hali ya uhalisia kuwa alikuwa anaumia juu ya kuhitaji penzi la Mariana!

“Unasena umekaa ndani ya moyo wangu?” Mariana akamuuliza huku akicheka kidogo.

“Ndiyo, nafikiri umenielewa. Nina maana kuwa nimekupenda, na ninaomba tuunganishe uhusiano wa karibu wa kuwa kitu kimoja. Au unasemaje?”

“Nimekuelewa unachosema. Mimi ni mtu mzima ambaye nina maamuzi yangu, na hata mimi nilipokuona mara ya kwanza, kuna ishara fulani ilionekana mwilini mwangu. Kama utakuwa mwaminifu, mimi sina shida, ukizingatia umri unazidi kukimbia…”

“Na kweli, kama utanikubali litakuwa jambo la heri…”

“Lakini kabla ya makubaliano ya kuungana kimahusiano, napenda kujua unaishi wapi?”

“Mimi kama nilivyowahi kukwambia, ninaishi eneo la Mwenge, umbali wa mita mia moja kutoka Barabara ya Shekilango, ambapo nimejenga nyumba yangu ndogo. Ninaiishi na mdogo wangu aitwaye Boniface, nafikiri umenielewa…”

“Ndiyo, nimekuelewa. Mimi ninaishi Kinondoni, mtaa wa Wema. Ninaishi na familia yetu, wazazi wangu, pamoja na ndugu zangu.”

“Kumbe bado unaishi nyumbani na wazazi wako?”

“Ndiyo, bado sijaachana nao. Baba yangu ni mkali sana, kwani hataki watoto wake wajiingize katika masula ya umalaya.”

“Umesema baba yako ni mkali sana?”

“Sana, tena hivi karibuni ameshawatimua dada zangu wawili kutoka pale nyumbani baada ya kwenda kinyume cha matakwa yake!”

“Ina maana walimuudhi sana?”

“Ah, si sana. Isipokuwa ni kama hivi kuwa na uhusiano na wanaume bila kuwashirikisha wazazi, kitendo ambacho baba alikiita ni umalaya!”

“Oh, pole sana. Kumbe na wewe unaweza kujiingiza katika matatizo ukiwa na uhusiano na mimi?”

“Ni kweli, ninaweza kupata matatizo, lakini inabidi kuwa makini sana. Tusikutane katika anga za baba.”

“Nashukuru sana kwa kuniambia ukweli huo, na kama nilivyokwambia tokea mwanzoni. Ninapendelea uhusiano wa kweli na wewe, na wala siyo kuharibiana maisha na ikiwezekana ni kuwa wachumba na hatimaye kuja kufunga pingu za maisha.”

“Hata mimi nitashukuru tukiwekeana ahadi ya kuoana na siyo ya kuchezeana na mwishowe kutupana!”

“Amini kuwa ninachokueleza Mariana, mimi nakupenda, na wala sifanyi masikhara.”

“Kama ni kweli umedhamiria, na mimi najipanga na kuweka akilini kuwa nina mchumba. Nikisema hivyo nina maana kuwa hata kama kuna mtu mwingine anayenisumbua niachane naye, umenipata?”

“Nimekupata, ni kweli ufanye hivyo. Mimi niko wazi kwa kila ninachosema!”

Fred  na Mariana waliendelea na maongezi yao, huku pia wakila na kunywa. Kwa muda wote ule wakawa wamezoeana kama watu waliokuwa na uhusiano wa muda mrefu, ambapo baada ya kutosheka, waliamua kuondoka pale Amazon Hotel.

Walitoka hadi nje ya hoteli ile, ambapo palikuwa na teksi chache zilizokuwa zimeegeshwa katika eneo maalum la maegesho. Fred alikodi teksi, ambayo iliyowachukua wote wawili, kuwapeleka majumbani kwao.

Alimpitisha Mariana nyumbani kwao, Kinondoni, mtaa wa Wema, na yeye ikampaleka nyumbani kwake, Mwenge. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa mapenzi yao, ambayo yalimea kwa kasi!

        *******

Hatimaye Fred alikuja kulewa penzi changa la mwanadada, Mariana, kiasi kwamba alikuwa na hamu ya kumuona mara kwa mara kwa kuhofia kunyang’anywa na wanaume waliokuwa na uroho, ambapo walikuwa tayari kuhonga kiasi chochote cha fedha ili kukamilisha malengo yao.

Baada ya mwezi mmoja hivi, Fred aliamua kufunga safari, kwenda nyumbani kwa akina Mariana, mtaa wa Wema, Kinondoni, kwa mara ya kwanza. Wakati huo, alikuwa bado anaishi nyumbani kwa wazazi wake, hivyo kufanya wawe wasionane mara kwa mara.

Wivu mkali ulikuwa umemtawala Fred, hivyo akasahau kile alichowahi kuambiwa na Mariana, kuwa, baba yake mzazi alikuwa mkali kama pilipili. Siku hiyo ya Jumapili, Fred alikodi teksi kutoka nyumbani kwake, Mwenge, na kuelekea Kinondoni. Kwa vile alikuwa anapafahamu, akamwambia dereva amshushe katika mtaa wa Wema.

Baada ya teksi ile kumshusha, yeye akajisogeza kando karibu na maduka kadhaa yaliyokuwa katika eneo lile. Halafu akampigia simu Mariana, na kumwambia kuwa yuko pale, hivyo aende. Na kweli, baada ya dakika tano hivi, Mariana alifika pale alipokuwa amesimama.

“Oh, Fred…” Mariana akasema huku akimpa mkono.

“Mariana…” Fred naye akasema.

“Vipi, mbona umekuja mpaka huku?” Mariana akamuuliza.

“Kwani hupendi nikutembelee?” Fred akamuuliza.

“Siyo sipendi unitembelee Fred…”

“Isipokuwa?”

“Baba mkali sana!” 

“Kwani yupo?”

“Hapana, ametoka kidogo.”

“Basi, usihofu. Mimi sina nia mbaya, nataka kukuoa kabisa, hivyo siyo mbaya kufika kwenu!”

“Najua hayo Fred, lakini kuna utaratibu wake wa kuja hapa nyumbani…” mariana aliendelea kumwambia Fred.

“Yote naelewa sana, lakini ni mapenzi tu ndiyo yanayonisumbua…”

“Haya, karibu sana…” mariana akamwambia.

Fred na Mariana walitofautiana kwa muda, halafu wakakubaliana, na akamkaribisha Fred nyumbani kwao, ikiwa ni mara ya kwanza. Baada ya kufika, alitambulishwa kwa mama yake mzazi, Bi. Salome Minja, pamoja na ndugu mwingine, kaka yake, Onesmo. 

Lakini siku ile ya Jumapili alipofika Fred, baba yake, mzee John Kwayu hakuwepo, kwani alikuwa katika mihangaiko yake ya kibiashara ambayo ilikuwa inamuweka bize sana. Mara nyingi alikuwa katika moja ya maduka yake yaliyoko eneo hilo la Kinondoni, ambayo huyasimamia mwenyewe.

Hata hivyo kufika kwake pale, kuliwachanganya sana mama yake na Mariana mwenyewe, hasa ukizingatia jinsi mzee John Kwayu alivyokuwa mkali sana, aliyekuwa anawachunga watoto wa kike, kwa kile alichodai kuwa hataki kudhalilishwa kwa kuletewa mimba isiyokuwa na wenyewe! Ni mpaka watakapopata wachumba na kuolewa, basi!

Kwa kumbukumbu tu, ni kwamba, mzee John Kwayu, baba yake Mariana, aliwahi kumfukuza mtoto wake wa kwanza, dada yake Mariana, aitwaye, Prisca. Yeye aliwahi kukutwa amesimama na mwanaume njiani, wakiwa katika mazungumzo yanayohusiana na mapenzi, kitu ambacho mzee yule hakukipendelea kabisa.  

Baada ya kumfukuza, Prisca aliamua kwenda kupanga chumba katika eneo jingine, ikiwa ni njia ya kumkimbia baba yake huyo, ambaye walimwona kama alikuwa akiendekeza mambo ya kizamani kwa kuwafuatilia watu wazima, waliokuwa wanajua jema na baya.

Hivyo basi, Prisca alipokwenda kupanga chumba, mzee Kwayu hakumfuatilia tena akimwacha na uhuru wake. Hata hivyo, kijana yule aliyekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Prisca, alifanya mipango ya kujitambulisha na mipango ikafanyakika na hatimaye wakaoana na kuendelea na maisha yao ya ndoa huko walipokuwa wanaishi.

Mzee Kwayu akabakiwa na watoto watatu aliokuwa anaishi nao pale nyumbani, ambao ni, Martina, Mariana na kijana wa kiume, Onesmo, ambaye alikuwa akisimamia miradi ya baba yake, maduka yaliyopo Kinondoni.

Hata hivyo, jinamizi liliendelea kuikumba familia ya mzee Kwayu, kwani mtoto wake mwingine, Martina, ambaye ni mtoto wa pili, aliyemfuata Prisca, naye alianza mahusiano ya siri na kijana mmoja aliyekuwa anaishi huko Masaki, Oysterbay, ambaye alikuwa ni mtoto wa kigogo mmoja mkubwa.

Baada ya kuzipata habari zile, mzee Kwayu akawekewa siku yake. Hata hivyo katika subira yake, hatimaye Martina alipata mimba akiwa shuleni kidato cha tatu. Akiwa na mimba yake, alifukuzwa na kukimbilia kwa huyo mwanaume aliyempa mimba hiyo, ambaye hata baba yake, hakutaka kumshtaki kwani alikuwa mtoto wa mkubwa!

Mwanaume huyo alimpokea Martina na kuishi naye mpaka alipojifungua salama mtoto wa kiume, hatimae mwanaume huyo akamsomesha Martina hadi kidato cha sita, na alipomaliza alimtafutia kazi ya maana katika benki moja wapo jijini.

Baada ya kuishi naye kwa muda, ndipo mwanaume huyo alipojitambulisha kwa wazazi wake na mpangilio wote wa mahari na vinginevyo ukafanyika na Martina akaolewa katika harusi kubwa iliyokuwa gumzo.

        ********

Kwa njia moja ama nyingine, mzee John Kwayu aliona kuwa msimamo wake wa kudhibiti watoto wake wa kike ulikuwa umefanikiwa. Basi, kati ya majanga yaliyowapata dada zake Mariana, yalimkuta punde tu baba yake aliporudi.

Alipata habari kuwa alikuwa amempeleka mwanaume pale nyumbani. Mariana aliitwa mara moja na kuulizwa juu ya tuhuma zile zinazomkabili!

“Mariana!” Mzee Kwayu alimwita mara baada ya kufika mbele yake.

“Bee,” Mariana aliitikia.

“Nimepata habari kuwa umemleta mwanaume hapa nyumbani, ni kweli?”

“Ni kweli baba,” Mariana alimwambia.

“Huyo mwanaume ni nani?”

“Ni mchumba wangu ambaye anataka kunioa baba…”

“Unasema mchumba?”

“Ndiyo baba.”

“Mbona mnapenda kunidhalilisha?” Mzee Kwayu aliuliza na kuendelea. “Hivi unajua taratibu za uchumba?”

Mariana akanyamaza akimya!

“Uchumba unataratibu zake, siyo wanaume kujiendea ovyo nyumbani. Na kuanzia sasa hivi sitaki kusikia jambo kama hili tena!”

“Sawa, baba,” Mariana alijibu huku akimwona kama baba yake alikuwa anatumia udikteta katika kuwachagulia anachotaka yeye!

“Haya, niondokee hapa nisije nikakupiga bure!” Mzee Kwayu akamwambia Mariana, ambaye aliondoka mara moja!

Hata hivyo, mbali ya kuambiwa yale na baba yake mzazi, Mariana hakumtahadharisha mpenzi wake Fred,  juu ya kile alichoambiwa na baba yake. Hali hiyo ilimfanya amtembelee mara kwa mara kila alipojisikia kufanya hivyo.

Anapofika, huwa wanatoka na kwenda kuburudika katika maeneo ya burudani katika eneo lile la Kinondoni na kwingineko. Habari za kufika kwa Fred, mzee Kwayu alikuwa anazipata wakati akiwa katika biashara zake.

Mzee Kwayu hakumsemesha Mariana, bali alisubiri mpaka siku atakayowakuta wakiwa wawili, ndipo awape kilichoko rohoni mwake, na ndipo siku nyingine Fred alifika tena nyumbani kwa akina Mariana kitu ambacho kilimfanya Mariana aogope sana!

Ilikuwa ni hatari sana ukizingatia alikuwa hajawahi kumtahadharisha Fred kwamba alikuwa hatakiwi pale nyumbani, hasa baba yake mzazi. Na bahati mbaya zaidi, alimkuta mzee Kwayu, ambaye alimpokea kwa maswali ya kipolisi, ambayo yalimtisha Fred.

“Karibu kijana!” Mzee Kwayu alimwambia Fred huku amemkazia macho yake makali!

“Ahsante mzee, nimekaribia…” Fred alisema.

“Tukusaidie kijana…”

“Samahani mzee, namuulizia Mariana, sijui yupo?” Fred aliuliza kwa nia nzuri, na hakujua kama mzee yule alikuwa anamtafuta kwa hamu!

“Mariana ni nani kwako?” Mzee Kwayu alimuuliza.

“Ni rafiki yangu tu…”

“Wewe si ulifika hapa Jumapili moja, na nilipomuuliza akasema wewe ni mchumba wake?”

“Ndiyo mzee…”

“Sasa urafiki na uchumba wapi na wapi?”

Fred alinyamaza kimya. Hakuwa na kusema.

“Sikiliza kijana,” Mzee Kwayu akamwambia. “Hapa umepotea njia, tafadhali sitaki kukuona tena hapa nyumbani kwangu. Kama unataka kuchumbia, fuata taratibu zinavyokwenda!”

Hakika Fred aliona kama alikuwa amethalilishwa sana na mzee Kwayu. Hivyo akiwa amechukia, aliondoka pale nyumbani kwa akina Mariana, bila hata kuonana naye ingawa waliwasiliana kwa simu.

Baadaye alipokutana na Mariana, alimsimulia yote, na kumwambia kuwa asingeweza kufika tena nyumbani kwao kwa jinsi alivyodhalilishwa na mzee Kwayu. Hata hivyo uhusiano wao wa kimapenzi uliendelea na kukolea ingawa palikuwa na kizuizi kile.

Ukweli ni kwamba Mariana alikuwa akimpa moyo Fred kwa kumwambia kuwa asiwe na wasiwasi, na hiyo yote ni kwa sababu alikuwa amekolea katika penzi la kijana yule mwenye kujipenda!

********

Pilikapilika za mzee Kwayu hazikuishia pale. Alizidi kuwa mkali dhidi ya huyo binti yake, Mariana kwa kile alichokiita kwenda kinyume cha maadili, kitu ambacho kilikuwa kinamdhalilisha mbele za watu. Kamwe hakupenda kunyooshewa kidole kwa ajili ya upuuzi unaofanywa na binti zake!

Hadithi hii imewahi kuchwapwa na gazeti la Mwananchi na Swahili Hub ni kitengo ndani ya Mwananchi.

Author: Gadi Solomon