Methali za Kiswahili na maana zake

Amani Njoka-Swahili Hub

Asiyesikia la mkuu, huvunjka guu: methali hii ina lengo la kuwatahadharisha watoto au vijana wadogo kuheshimu yale wanayoambiwa na wakubwa zao. Sababu kuu ya kufanya hivyo ni kwa sababu watu wazima wanatajiriba ya maisha na hivyo maelekezo yao huwa ni msaada kwa vijana wadogo na endapo wakiipuuza wanaweza kujikuta katika matatizo.

Abebwaye hujikaza: huwakumbusha watu wajibu wa kufanya juhudi za kujisaidia wenyewe pale wanapopewa msaada wa awali. Ikiwa utasaidiwa basi abgalau onesha juhudi za kujiweza pindi msaada utakapofika mwisho

Akili ni nywele kila mtu ana zake: hutukumbusha kuwa kila binadamu ana mawazo na mtazamo wake wa kufanya au kuamini mambo hivyo uono hakutafanana na mwingine.

Aisifuye mvua, imemnyea: kila jambo ambalo mtu analizungumzia atakuwa aidha na uzoefu nalo au kwa namna moja ama nyingine analifahamu.

Asiefunzwa na mama, huvunzwa na ulimwengu: maonyo ya wazaz, walezi au watu wazima yana nafasi kubwa katika ustawi wa maisha ya vijana, hivyo ni muhimu kuwasikiliza lakini ikitokea maonyo hayo hayasikilizwi basi watajifunza mambo mabaya kutoka kwa watu wengine na yataleta madhara. Vilevile hutukumbusha kuwa wazazi wanaweza kukuadhibu kwa wema tena kwa upendo lakini watu wengine watakuadhibu bila huruma endapo utakosea.

Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe: hukumbusha kuwa hatuna budi kuwaadhibu au kuaonya watoto au watu wanapokosea pindi wanapokosea kabla hawajakomaa katika yale yasiyofaa kwani tutawapoteza.

Bandu bandu humaliza gogo: kufanya jambo kidogokidogo hutufanya tuwe na mazoea ambayo yanaweza kuleta madhara au yasilete.

Harakaharaka haina baraka: ni sharti tufanye mambo kwa utaratibu na kwa usahihi. Kufanya mambo kwa uharaka usababisha yasifanyike kwa usahihi unaohitajika.

Baniani mbaya kiatu chake dawa: kila jambo, kitu au mtu ana mbaya, matata au anayeonekana ni mgumu basi ana mbabe wake au suluhisho lake.

Bora nusu shari kuliko shari kamili: ni vyema kulitatua jambo au changamoto ikiwa ndogo kwa sababu ikiwa kubwa italeta madhara zaidi. Ni sawa na kusema usipoziba ufa utajenga ukuta.

Chovya chovya humaliza buyu la asali: rejea Bandu bandu humaliza gogo.

Baada ya dhiki faraja: kila wakati mgumu ambao mtu anapitia utaisha na utakuja wkati wa raha, hukumbusha kufanya kazi kwa bidii katika mazingira yoyote kwani baadaye matunda yataonekana na kustarehe. pia, fanya kazi kama mtumwa ule kama mfalme.

Chanda chema huvishwa pete: kila mtu anayefanya vyema hupongezwa, kila kitu kizuri hutunzwa.

Damu nzito kuliko maji:ndugu wanaoneana hruma na uchungu zaid kuliko wasio na udugu. Uchungu au huruma hizo huenda mbali zaidi kwa kumtetea mtu hata kama ana makosa kwa sababu tu ni ndugu.

Hakuna marefu yasiyo na ncha:jambo lolote lile lina mwisho wake haijalishi ni baya au ni zuri. Hutukumbusha kuwa nyakati tulizo nazo zina mwisho hivyo ni vyema wakati uliopo utumike vyema

Fimbo ya mbali haiui nyoka:msaada pekee ni ule uliopo karibu na wewe wala si ule uliopo mbali, jambo lolote likikupata ni vyema ukawashirikisha watu wa karibu . Wakati mwingine watu hutafuta suluhisho na tatizo kwa watu wa mbali au lenye gharama badala ya ile aliyonayo.

Asiyekubali kushindwa si mshindani: jambo likikushinda kubali kuwa limekushinda au ikiwa mlikuwa mnashindana na ukashinwa basi ukubali kwa kuwa siku zote mshindi huwa ni mmoja na hii itakupa wakati zuri wa kujipanga upya ili wakati mwingine ushinde.

Dalili ya mvua ni mawingu:kwa kawaida mvua ikikaribia kunyesha wingu zito hutanda . Manake ni kwamba kabla jambo halijatokea huwa na dalili, wakati mwingine hata ugonjwa huwa na dalili na hivyo wahusika kujiandaa kwa namna yeyote kutegemeana na jambo kama ni ala heri au shari.

Dawa ya moto ni mto: methali huhamasisha watu kusimama kujitetea au kuchukua hatua kukabiliana na jambo hasa kwa kutumia nguvu. Mara nyingi humtaka mtu alipize, ikiwa kapigwa basi na yeye apigane.

Dunia tambara bovu: ulimwengu una mambo mengi maovu kulingana na binadamu ambavyo wamebadilika. Mambo mengi mabaya yameibuka na hata usalama umekuwa mdogo. Hivyo methali hii hutumika kuwakumbusha watu kuwa na tahadhari kubwa.

Author: Gadi Solomon