Mfahamu Mwandishi wa Mashairi ya Wasakatonge

Umbuji ni kijiji kiliopo pembezoni mwa Wilaya ya Kati, Muhammed Seif Khatib alizaliwa usiku wa manane wa tarehe 10 Mei, 1952 majira ya vuli.

Dk Khatib alitoka kwenye ukoo wenye asili ya kusini ya Makunduchi na Jambiani.

Ndoa ya baba mzazi wa Seif Khatib na mama mzazi Tatu Kombo ilibarikiwa watoto wanne, wanawake wawili na wanaume wawili; Sijamini, Ali, Muhammed (marehemu) na kitindamimba Maimuna (marehemu). Seif alioa mke mwingine na kubarikiwa mtoto mwanamke aitwaye Rukia (marehemu).

Mwandishi huyu ingawa alizaliwa kijijini lakini makuzi yake yalifinyangwa mjini. Alipata elimu yake ya madrasa katika chuo cha Bi. Mwanzena na badaye katika Msikiti Barza.

Elimu ya msingi alisoma Fuoni na Kiembesamaki. Hakufaulu kwenda sekondari. Alisomea Ualimu Nkrumah na kufundisha shule kadhaa za msingi ikiwemo Umbuji, Chaani, Darajani na Forodhani.

Mohammed muda wote hakutosheka na kiwango chake cha elimu. Alihangaika huku na huku, panda shuka hadi pale alipofanikiwa kuhitimu elimu ya sekondari ya kiwango cha kawaida na kuwa mtahiniwa wa faragha kwa sekondari ya kiwango cha juu.

 Baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975. Baada ya kusoma muda mfupi Chuo cha Uwalimu na Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni. Muhammed alibahatika kwenda Uingereza kusoma shahada ya uzamili School of Oriental and African Study ya Chuo Kikuu cha London mwaka 1981/2. Shahada ya uzamivu aliipata Chuo Kikuu cha Dodoma.

Aliingia katika siasa za vijana kwa miaka 10 (1978 – 1988). Miaka 23 iliyofuatia (1988 – 2010) akahudumu katika Serikali akiwa waziri wa mambo ya ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu – Habari na Siasa na baadaye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo. Pia aliwahi kujiunga katika nafasi za ubunge wa vijana na hatimaye kuwa mbunge wa jimbo la Uzini hadi 2015.

Kipaji cha usanii cha Muhammed kilihitaji kuibuliwa. Alikuwa mshiriki wa sanaa za mashairi tangu yupo skuli za msingi na kuwahi kutunga mashairi na kusomwa Sauti Unguja kwa wakati huo na sasa ni Redio ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC). Alipokuwa Chuo cha Ualimu alitunga mashairi ya nyimbo, kuweka sauti na hata kuimba Taarabu asilia. Ushiriki wake katika vikundi vya Taarabu ya Kikwajuni na Nadi Akhwani – Safaa kulipalilia kukua kwa kipaji chake cha ushairi.

Kazi yake ya kwanza iliyochapishwa ilikuwa ni Utenzi wa Ukombozi wa Zanzibar (1975) ikafuatia na Fungate ya Uhuru (1988), Pambazuko la Afrika (1982), Kipanga (Hadithi Fupi), Taarabu Zanzibar (1992), Wasakatonge (2016), Chanjo (2016) na Vifaru Weusi (2016).

Kudumu kwa kazi ya Fungate ya Uhuru na Wasakatonge katika utahini wa sekondari nchini Tanzania ni uthibitisho wa kazi nzuri sana ya ushairi wake. Kazi mbili hizi zilipata tuzo, Fungate ya Uhuru ilipata tuzo ya Shaaban Robert iliyotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Wasakatonge iliyotolewa na PATA (Jumuiya ya Uchapishaji Tanzania).

Dkt. Seif pia alikuwa ni mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza) hadi umauti wake ulipomkuta mwaka 2020.


MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU PEPONI – AMIN

IMEANDALIWA KWA MSAADA WA MTANDANO WA BAKIZA

Author: Gadi Solomon