Mfumo wa elimu ya Tanzania ni butu?

Na Benard Semen

Nini mtazamo wa Watanzania kuhusu mfumo wa elimu?

Sauti za Watanzania zinasikika kila mahala zikiulalamikia mfumo wa elimu ya Tanzania. Madai ni kwamba, mfumo wa elimu ya Tanzania haumuandai kisawasawa mwanafunzi kwani ni mfumo unaofundisha nadharia zaidi kuliko vitendo, baada ya wanafunzi kuhitimu kushindwa kujitegemea. Vilevile mfumo huu ni wa kikoloni hivyo umepitwa na wakati. Sambamba na hiyo, hata wahitimu wengine wanadai kuwa, elimu ya Tanzania ni ya makaratasi maana yake haina maana yoyote kwani hawawezi kuitumia maishani.

Mei, 2019 Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano akichangia mada katika Bunge la 11 Mkutano wa 15 alisema kuwa,  “elimu ya Tanzania siyo ufunguo wa maisha bali ni kifungo cha maisha, na mtoto aliyesoma ni kama kiazi kilichoshindwa kuiva, kwa sababu hawezi kufanya chochote. Kwa maana hiyo mtoto ambaye hajasoma ndiyo mwenye faida kwenye familia kuliko aliyesoma”. Kwa ujumla mfumo wa elimu unalalamikiwa na watu wengi na wa aina tofauti tofaouti wakidai kuwa ni butu.

Je, ni kweli mfumo wa elimu ya Tanzania ni butu?

Kwa hakika, mfumo wa elimu ya Tanzania ni mfumo bora na dhabiti ambao unapika vyema wanafunzi na kuzalisha watu wenye uwezo na utashi mkubwa ambao wanaleta mabadiliko makubwa katika jamii. Wapo Watanzania wengi ambao ni zao la elimu ya Tanzania ambao wamefanya mambo mazuri na makubwa kitaifa na kimataifa.

Kwa mfano, Mh. Dkt. Asha Rose Mtengeti Migiro, ambaye ni balozi wa Tanzania nchini Uingereza, ambapo alisoma hapauapa nchini Tanzania; alisoma shule ya msingi MnaziMmoja  na shule ya sekondari Weruweru. Vilevile, alisoma shahada ya awali na ya umahiri ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lakini amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa 2007 hadi 2012 na ndiye Mwafrika wa kwanza kushika nafasi hiyo na hajatokea mwingine mpaka leo.

Vilevile, Mh. Dkt. Philip Isdor Mpango, ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais, naye alisoma hapa Nchini Tanzania, ambapo alisoma Muyama shule ya msingi, Itanga sekondari na Ihungo sekondari. Vilevile, alisoma Shahada ya awali, shahada ya umahiri na shahada ya uzamivu ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini aliwahi kuwa Mchumi Mwandamizi (Senior Economist) wa Benki ya Dunia kati ya mwaka 2002 na 2006.

Hali kadhalika, Rebeca Gyumi, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji  wa Msichana Initiative, naye alisoma hapahapa Tanzania ambapo, alisoma Mazengo shule ya Msingi na Kilakala Sekondari na baadae alisoma shahada ya awali ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 2012. Binti huyu amewahi kupata tuzo ya United Nation Global Goals Award mwaka 2016 na tuzo ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa mwaka 2018 huko mjini New York, Marekani kwa sababu ya mchango wake mkubwa katika jamii. Kwa ujumla ipo mifano mingi ya watu mashuhuri ambao ni alama na tunu kubwa kwa taifa letu ambao ni zao la elimu ya Tanzania.

Licha wa kuwapo kwa mafanikio hayo, vilevile kuna watu kutoka mataifa ya nje ambao wanakuja Tanzania kusoma. Kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina zaidi ya wanafunzi 100 kutoka mataifa mbalimbali ya nje kama vile Ujerumani, China, Italia, Ufaransa, Uswizi, Pakistani, Misiri, Kenya, Uganda, Burundi, Nigeria, Kongo,  Ghana, Malawi na mataifa mengine ambao wanasoma shahada za awali, shahada za umahiri na shahada ya uzamivu katika kozi mbalimbali.

Mathalani, mtaala wa elimu unafanyiwa mabadiliko kila wakati. Kwa mfano katika mtaala wa shule za msingi wa mwaka 2005 na 2006 kulikuwa na masomo sita tu ambayo ni Kiswahili, English, Maarifa ya jamii, Sayansi, Hisabati na somo la stadi za kazi. Lakini katika maboresho mtaala huo ya mwaka 2012 na 2013 kukawa na masomo tisa ambayo ni Kiswahili, Hisabati, English na  Sayansi lakini somo la “Maarifa ya jamii” lilivunjwavunjwa na kuzaa masomo matatu ambayo ni Jiografia, Uraia na historia. Vilevile likaongezwa somo la Haiba na Michezo na pamoja na Tehama. Lakini katika maboresho ya mwaka 2018 na 2019 kukawa na masomo sita ambayo ni Kiswahili, English, Maarifa ya jamii, Hisabati, Uraia na maadili vilevile somo la sayansi limepanuliwa na kuitwa sayansi na teknolojia ambapo mwanafunzi atajifunza mambo ya kisayansi pamoja na tehama.

Kuwapo kwa hali hii inathihirisha kuwa, elimu ya Tanzania siyo mtuamo wala si butu kwa sababu ni elimu inayoendana na wakati, inazalisha watu mahiri na inawavutia watu wengine kutoka mataifa ya nje kuja kusoma.

Kwa nini mfumo wa elimu unaandamwa?

Mitazamo hasi ya Watanzania juu ya mfumo wa elimu imeibuka hivi karibuni, tatizo kubwa linalochochea ni ukosefu wa ajira. Kipindi cha nyuma wanafunzi walihitimu na kupata kazi hakuna aliyewahi kusimama na kusontea kidole mfumo elimu bali kila mtu alifanya juhudi kuipata elimu. Katika kipindi hiki watu wanaona hakuna maana ya kusoma kwa sababu baada ya kuhitimu hukuna kazi. Kwa kweli tatizo hili ni kubwa katika nchi ya Tanzania na linawasumbua.

Lakini tunapaswa kujua kuwa mfumo wa elimu unajikita zaidi kuzalisha wasomi na siyo kuajiri, elimu ubora na ukosefu wa ajira ni kama kichwa na kofia unaweza kuvaa au usivae. Afrika Kusini inatajwa kuwa nchi ya kwanza yenye ukosefu wa ajira duniani lakini inatoa elimu bora zaidi kuliko nchi zingine barani Afrika. Kwa mfano takwimu za vyuo vikuu bora Afrika za mwaka 2022 zinabainisha vyuo vikuu vitatu bora Afrika zinatoka Afrika Kusini, ambacho chuo kikuu cha Cape Town kinashika nafasi ya kwanza, chuo kikuu cha Stellenbosch kinasikika nafasi ya pili, na  chuo Kikuu cha Witwatersrand kinashika nafasi ya tatu.

Nini kifanyike?

Ijapokuwa yapo mataifa mengine mengi yaliyoathirika zaidi tatizo la ajira, lakini haimaanishi kwamba taifa la Tanzania  hata likiathirika litakuwa salama. Kwa hakika ni fahari kubwa kwa taifa kuwa na watu wasomi ndio maana Baba wa Taifa Hayati J.K.Nyerere alisema “Tanzania tunao maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini ” hivyo katika ujenzi wa taifa la leo na la kesho ni muhimu kuthamini wasomi na kuwajali. Katika kunusuru tatizo hili serikali inapaswa kuwa mstari wa mbele.Wakati serikali inazidi kubuni mikakati ya kutatua tatizo hili napendekeza mbinu kadhaa ambazo ni kheri kuzingatiwa katika maboresho, ambazo ni:-

Mosi, kuwepo kwa tuzo za vijana.

Taifa la Tanzania linao vijana wenye uwezo na ujuzi mkubwa lakini wanakosa njia ya kuanza na molari ya kuendelea; ili kuwasaidia vijana hao serikali inapaswa kutambua mawazo yao na uwezo wao kwa kuwapa tuzo maalum. Katika tuzo hizo inapaswa itengwe fedha kwa walioshinda tuzo, aghalabu milioni 40 kwa mshindi wa kwanza katika nyanja husika. Aidha, kuwapo na tuzo za vijana wenye taasisi au makampuni binafsi, tuzo za vijana wenye ubunifu, vipaji n.k hii itachochea kuwapa moyo wa uthubtu vijana wengine wenye mawazo bunifu na kuwafanya kuwa na jitihada zaidi katika kukuza mawazo yao. Kwa mfano Bongo Star Search (BSS) imeweza kusaidia vijana wengi kuziishi ndoto zao kupitia tuzo. Hivyo tunapaswa kuwa na BSS katika sekta zote.

Pili, kuwepo kwa mikutano na mafunzo maalumu ya vijana wenye ubunifu.

Ni jambo la kheri kukiandaliwa kwa mikutano mikubwa ya kitaifa ya vijana, mikutano hiyo iwe ya bure, vijana walipiwe nauli na chakula na kuwepo na posho ili vijana wahamasike na wapate kushiriki. Hii itasaidia kuwakutanisha vijana na watu waliofanikiwa zaidi, wenye uwezo, ubunifu na uzoefu ili waweze kujifunza zaidi na kubadilishana mawazo. Hii itawasaidia kukuza ujuzi, maarifa na kuongeza uzoefu. Hali kadhalika kuwepo na mafunzo maalumu kulingana na uwezo wao aidha mafunzo ya uongozi, ujasiriamali, sanaa n.k. Vilevile vijana waelezewe fursa zinazopatikana kulingana na maarifa yao na namna ya kuzifikia. Kwa hakika wahitimu wengi wana uelewa mdogo juu ya fursa na namna ya kuzifikia, sababu hii inasababisha vijana kukosa fursa. Kwa mfano Ofisi ya waziri mkuu kazi, vijana ajira na watu wenye ulemavu kupitia Tanzania Employment Service Agency (TaESA) inatoa fursa mbalimbali za kazi lakini ni wahitimu wachache wenye ufahamu.

Tatu, wahitimu kupewa mshahara ili kuweza kujikimu.

Hali ya wahitimu nchini ni mbaya, wengi wamekosa tumaini kwa sababu ya hali ngumu ya maisha. Hali hii inasababisha matatizo mbalimbali kuibuka, mathalani wasomi wengi kujihusisha na biashara haramu, kufanya mambo ya kiharifu na yasiyofaa katika jamii. Kitendo hiki kinapoteza nuru ya taifa, hivyo ni muhimu kuwatazama kwa jicho la kipekee. Februari 15, 2022, Rais wa Algeria Mh. Abdalmadjid Tebboune alisema, wahitimu nchini humo watakuwa wanapokea robo tatu ya kima cha chini cha mshahara wanaopoke wafanyakazi. Hivyo hata nchini Tanzania ni jambo la busara likitengwa fungu kwa ajili ya wahitimu ambao hawajapata kazi inayoeleweka. Kufanya hivyo itasaidia kupunguza ukali wa maisha na kuchochea maendeleo katika jamii.

Nne, kuongeza mwaka mmoja wa kusoma vyuo na vyuo vikuu.

Kuna haja ya kuongeza mwaka mmoja wa muda wa kuhitimu ngazi ya astashahada, stashahada na shahada, kwa mfano mwanafunzi anasoma miaka 2, 3, 4 au 5 uongezeke mwaka mmoja; mwaka huo uwe wa mafunzo kazini (Internish) ambapo mwanafunzi atafanya kazi kwa mwaka mmoja na atalipwa mshahara kila mwezi kama mwajiriwa ila yasiwepo makato yoyote kama vile makato ya NSSF, Bima ya Afya, HESLB n.k. Baada ya mwaka mmoja kuisha mwanafunzi atarudi chuoni kwake na kupata cheti. Hii itasaidia wanafunzi kupata uzoefu wa kazi, kuonyesha uwezo na ujuzi wao vilevile kupata kiasi cha kuanzia maisha. Kwa mfano kwenye kada ya afya, mwanafunzi wa shahada ya awali akimaliza masomo yake aidha miaka mitatu au mitano mwaka mmoja huongezeka mbele kwa ajili ya  mafunzo kazini. Hali hii inapaswa kuwa katika kozi zote na kwa ngazi zote.

Yangu ni hayo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Benard Semen

+255 621 406 438

semenbenard95@gmail.com

Author: Gadi Solomon