Milango ya Kiswahili yafunguliwa rasmi SADC

Kelvin Matandiko, Mwananchi
kmatandiko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Milango ya fursa kwa wasomi wa lugha ya Kiswahili imeendelea kufunguka zaidi baada ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) ulioanza kuanza majadiliano ya kuwezesha lugha hiyo ianze kutumika katika nyaraka na shughuli zote za kisekta.

Katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi SADC Agosti mwaka jana, lugha ya Kiswahili ilipitishwa rasmi kutumika ngazi ya vikao vya wakuu wa nchi na baraza la mawaziri, sawa na lugha ya Kireno, Kifaransa na Kiingereza.

“Sasa imeamuliwa rasmi itumike ngazi ya kisekta na katika nyaraka zote za SADC, hii ni hatua ya kujivunia kama watanzania,”amesema Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipozungumza na wanahabari leo Machi 12,2021

Kikao hicho kwa njia ya mtandao kimehusisha mawaziri wa mambo ya nje wote kutoka nchi 16 za SADC chini ya mwenyeji wake Msumbiji.

Hatua hiyo inajitokeza wakati tayari wizara yenye dhamana na lugha ya Kiswahili ikiandaa kanzi data ya kukusanya na kuwatambua watalaamu wa lugha hiyo kwa ajili ya kuwatafutia masoko.

Author: Gadi Solomon