Mimi nakataa

 1. Kwa kweli ile sauti,
  mjini ilotangaa
  kwamba tusile chapati
  piya nyingine bidhaa
  kwangu ni suala nyeti,
  na tena ninashangaa
  kisa ni yule jamaa
  mimi mtanisamehe
 2. Siachi kula andazi,
  na chapati za kung’aa
  unga wala siulizi,
  nikipewa nitatwaa
  hilo jambo siliwezi
  niache vyakunifaa
  kisa ni yule jamaa
  mimi mtanisamehe
 3. Siwezi kuacha kazi,
  penzi hilo kwangu laa
  wana wakose mavazi,
  wavalishwe vitambaa
  niyakose matumizi
  eti ndio ushujaakisa ni yule jamaa
  mimi mtanisamehe
 4. Siungi hayo maneno
  kipembeni ninakaa
  nipewe kilo ya ngano
  nijidai kushupaa
  hili siungi mkono
  hafanyi hata kichaa
  kisa ni yule jamaa
  mimi mtanisamehe
 5. Tuzisuse biashara
  kisa yule kuambaa
  kwangu hii si busara
  suseni mie nakaa
  mawazo haya si bora
  yatupwe yana kinyaa
  kisa ni yule jamaa
  mimi mtanisamehe
 6. Tamati ya beti sita
  nawaaga ulamaa
  mimi siachi mafuta
  wala sitoacha mbaa
  hili halikunivuta
  uadui tunazaa
  kisa ni yule jamaa
  mimi mtanisamehe.

Author: Gadi Solomon